Saturday 25 November 2017

Shambulio la Msikiti laua 235 Misri




Wanamgambo wametekeleza shambulio la bomu na ufyatuaji wa risasi katika msikiti mmoja uliopo kaskazini mwa eneo la Sinai na kuwaua takriban watu 235 kulingana na chombo cha habari cha taifa.

Walioshuhudia wanasema kuwa msikiti wa al-Rawda katika mji wa Bir al-Abeid , karibu na al-Arish ulilengwa wakati wa ibada ya Ijumaa.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa wanaume wanne waliokuwa ndani ya gari moja waliwafyatulia risasi waliokuwa wakiabudu kulingana na chombo cha habari cha AP.

Misri imekuwa ikikabiliana na wanamgambo katika eneo hilo tangu 2013.
Kumekuwa na mshambulio ya mara kwa mara yanayolaumiwa kutekelezwa na wanamgambo katika rasi ya Sinai lakini hilo ni shambulio baya zaidi kuwahi kufanyika.

Ripoti moja inasema kuwa waliolengwa ni wafuasi wa maafisa wa usalama waliokuwa wakitekeleza ibada katika msikiti huo.

Wakazi wa eneo hilo wanasema kuwa wafuasi wa madhehebu ya Sufi hukongamana katika msikiti huo.

Makundi ya wanajihad likiwemo lile la Islamic State wanawaona wasufi kama watu wasioamini.
Rais Abdul Fattah al-Sisi anatarajiwa kukutana na maafisa wa usalama kuzungumzia kisa hicho .

No comments:

Post a Comment