Thursday, 23 November 2017

Sukari ya viwandani yakwama bandarini Dar




Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) limesema sukari ya viwandani ya wanachama wake imekwama katika Bandari ya Dar es Salaam kwa wiki mbili sasa, jambo linaloweza kuathiri uzalishaji.

CTI imesema wanashindwa kuiondoa sukari hiyo baada ya kukosa kibali cha kufanya hivyo kutoka Bodi ya Sukari kwa kile kinachoelezwa kuwa ni agizo la Serikali kuzuia uagizaji wa bidhaa hiyo.

Hata hivyo, mtaalamu wa sera wa CTI, Akida Mnyenyelwa alisema agizo hilo halikulenga sukari hiyo inayotumika viwandani kuzalisha bidhaa za aina tofauti kama vile dawa na vinywaji baridi.

“Jambo kubwa linalosababisha sukari hiyo kukwama ni wahusika kushindwa kutofautisha kati ya sukari ya kawaida na ya viwandani. Kutokana na sukari hiyo kutozalishwa katika nchi zote za Afrika Mashariki (EAC), upo utaratibu wa kuiingiza ndani ya nchi wanachama tena kwa msamaha wa kodi. Nchini, hutozwa ushuru wa asilimia 10 tu,” alisema Mnyenyelwa.

Alisema kutokana na zuio hilo, baadhi ya viwanda vimekosa sukari kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa licha ya taratibu zote muhimu za kuingiza mzigo huo kufuatwa.

Mtalaamu huyo alisema uingizwaji wa sukari hiyo umefuata taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupata vibali vya uagizaji kwa ajili ya matumizi ya viwanda.

Taratibu zilizopo kukamilisha uingizaji wa sukari hiyo, Mnyenyelwa alisema, muombaji anatakiwa kupata ruhusa ya Bodi ya Sukari ambayo itapeleka taarifa zake Mamlaka ya Mapato (TRA) inayopitia orodha ya waombaji wote kabla ya kupeleka majina ya waliokidhi vigezo kwenye Sekretarieti ya EAC.

Alisema majina ya waombaji walioridhiwa na nchi zote wanachama wa EAC yakishapokelewa, huchapwa kwenye gazeti la jumuiya hiyo kisha kupata msamaha wa kodi kwa mujibu wa sheria.

Baada ya hapo, kila muombaji anaweza kuagiza mzigo kwa kadri alivyopendekeza na kukubaliwa kwenye maombi yake. Kwa waagizaji wa nchini, hupaswa kupata kibali cha Bodi ya Sukari kuwaruhusu kuiondoa bandarini.

“Huko ndiko tulikokwama. Bodi haijatoa vibali tangu Rais (John Magufuli) azuie uagizaji wa sukari. Tunaambiwa wameomba ufafanuzi ofisi ya waziri mkuu lakini mpaka sasa hawajajibiwa, hivyo sukari bado ipo bandarini,” alisema.

Miongoni mwa waagizaji ambao sukari yao imekwama, alisema ni Bonite Bottles iliyoagiza tani 650 na Nyanza Bottles yenye tani 1,450. Alisema kwamba kuendelea kubaki bandarini hapo kunaongeza gharama za utunzaji (storage) pamoja na tozo za bandari (demurrage charges).

“Uhakiki matumizi ya sukari hii ikishaingia hufanywa na TRA kujiridhisha kama inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Mnyenyelwa.

Februari mwaka jana, Rais Magufuli alipiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje ili kuvilinda viwanda vya ndani na kuagiza vibali vyote vya kufanya hivyo vitolewe na ama ofisi yake au ya waziri mkuu. Akiwa kwenye ziara wilayani Missenyi hivi karibuni ambako pia alitembelea kiwanda cha Sukari Kagera, alisisitiza kuwalinda wazalishaji hao.

Uongozi wa Bodi ya Sukari ulithibitisha kuwapo kwa changamoto za kutoa vibali vya kuondoa sukari hiyo bandarini lakini ukasema juhudi za makusudi zinaendelea kuhakikisha muafaka unapatikana.

“Jana (juzi) viongozi wa bodi wakiwa na wawakilishi CTI walikutana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Ndani ya siku mbili tatu hizi mambo yatakaa sawa,” alisema ofisa mmoja ambaye si msemaji wa bodi hiyo.

Kwa kutambua kero iliyopo, waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema atawaondoa wafanyakazi wote wanaokwamisha utoaji wa mizigo bandarini hapo kabla hajawajibishwa.

“Nitawafuta mmoja baada ya mwingine na kuna mtu mmoja anaitwa Khalid anashinda sana bandarini. Nitamtoa hata kama aliteuliwa na nani,” alisema Mwijage.

Alisema kwa hali ya Tanzania ilivyo sasa bado inaagiza bidhaa nyingi kutoka nje kuliko inazouza, hivyo ni lazima atengeneze mazingira mazuri yasiyo na vikwazo kutoka kwa watumishi wa idara hiyo nyeti.

Waziri huyo alisema hayo jana alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo matatu ya usambazaji bidhaa za kampuni ya NBMG kutoka China utakaogharimu Dola 75 milioni za Marekani (zaidi ya Sh165 bilioni).

No comments:

Post a Comment