Saturday 25 November 2017

Waziri Ummy ahimiza wananchi kuwa na Bima ya Afya



Waziri wa Afya,  Ummy Mwalimu amesema mrundikano wa wagonjwa wengi katika meli ya Wachina, umetokana na wananchi wengi kukosa bima za afya.

Kufuatia hilo Ummy ametoa siku 60 kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuhakikisha wanaanza kutoa bima za afya kwa watoto za kulipa kidogokidogo,  huku akiwataka kuongeza idadi ya wanachama.

Ameyasema hayo leo Novemba 24 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi kadi za bima ya afya, vyeti vya kuzaliwa na kadi za benki kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

"Ile meli ya Wachina watu wamejazana pale maana yake watu hawawezi kufikia gharama za matibabu na ndiyo maana wanakwenda kule ni bure, kama watu wana bima huna haja kusubiri meli ya Wachina mtu anakuja Muhimbili lakini watu wanasubiri vya bure," amesema.

Amesema mfuko huo unapaswa kuunganisha watu na kulipa kidogokidogo ili kila mwananchi aweze kupata kadi ya matibabu itakayomuwezesha kutibiwa kwa wakati.

Amesema alishawaambia NHIF kuanzisha fao la wajawazito kujifungulia popote, ambapo amewataka walikamilishe kabla hajawasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni.   

Ametoa rai kwa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya huku akiitaka mifuko mingine ya bima za afya kutengeneza mazingira rahisi na yenye bei za kiushindani ili kuvutia watu kujiunga.

"Mimi mtu akiwa tayari kutengeneza fao la watoto nipo tayari kwa hospitali zetu na hata kadi za mama na mwana,  wakina baba hawatashindwa kuchangia 50400 hadi mtoto atakapofikisha mwaka mmoja haiwezekani," amesema.

Ametoa wito kwa wazazi, walezi kuhakikisha watoto wao wanakuwa na uhakika  wa matibabu  kabla ya kuugua kwa kumkatia kadi ya bima ya afya  ya sh50400.

No comments:

Post a Comment