BAADA ya uwepo wa taarifa za wavuvi wilayani Rorya Mkoa wa Mara kuvamiwa na kunyang’anywa zana zao za kazi na samaki na maharamia wakiwa majini ndani ya Ziwa Victoria, wito umetolewa kwa Serikali kupitia Jeshi la Polisi kitengo cha majini kuimarisha ulinzi.
Wito huo ulitolewa na wananchi mbalimbali wanaojishughulisha na uvuvi katika Ziwa Victoria wilayani hapa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, kukagua hali ilivyo.
Mmoja wa wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi katika mwalo wa Nyang’ombe uliopo Kata ya Nyamagaro wilayani hapa, Richard Marwa, akizungumza kwa niaba ya wenzake alimwambia Naibu Waziri kwamba wanateseka sana wakati wakitekeleza shughuli zao kutokana na majambazi kutoka nchi jirani ya Uganda kuwapiga na kuwanyang’anya samaki.
“Tunaiomba Serikali kuingilia kati suala hili la wavuvi wa Tanzania kuvamiwa na majambazi kutoka nchi jirani ya Uganda huku wakitunyang’anya samaki na kutupiga na wengine hata kuuawa,” alisema Marwa.
Suala hilo liliongezewa uzito na Mbunge wa Jimbo la Rorya, Lameck Airo (CCM), ambaye alisema tatizo hilo ni la muda mrefu ambapo aliiomba Serikali kusikia kilio cha wananchi wake kwa kuongeza ulinzi ndani ya Ziwa Victoria ili kuondoa kero hiyo.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Polisi Wanamaji Shirati Wilaya ya Rorya, Yusuph Juma, alisema kikosi chake kinazidiwa kwa sababu hawana vifaa vya kutosheleza mahitaji na vilivyopo havifanyi kazi kutokana na kukaa muda mrefu bila kutumika.
Akijibu hoja hizo za wananchi, Naibu Waziri, Mhandisi Hamad Masauni, alisema Serikali ipo katika mashauri kuhakikisha ulinzi wa majini unaimarishwa kupitia Jeshi la Polisi huku akiahidi kukitafutia boti nyingine kikosi cha wanamaji Shirati ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao.
“Tumekubaliana kuwaombea boti itakayokuwa na uwezo wa kwenda zaidi ya kilomita 20 kwa saa ili kuimarisha ulinzi majini hususani kwa wavuvi w
No comments:
Post a Comment