Yamkini umeshawahi kusikia kwamba wanaume hukosa uaminifu kwa sababu za kimwili zaidi wakati wanawake nao hukosa uaminifu kwasababu za kihisia.
Nikweli kuwa upo ukweli katika hilo, ingawa katika utafiti huu wanawake mbalimbali walipoulizwa kwanini walijiingiza katika mahusiano yasiri mbali na wapenzi wao walikuwa na sababu tele zakuelezea, wako walioelezea kuwa walikuwa wanafurahisha hisia zao tu na wengine walikuwa kwenye mkakati wakulipiza kisasi kwa kile walichowahi kufanyiwa na wapenzi wao, na sababu nyingine nyingi zilielezwa.
Jaribu kusoma kwa umakini ili ufahamu nini walikisema na kilichowafanya kujiingiza katika majaribu hayo. Ni matumaini yangu kwamba utakutana na sababu nyingine ninazokusibu au zilizowahi kukusibu wewe, na yamkini pia ukapata kufahamu kwanini mambo fulani yanaendela vile yalivyo.
Kukosekana kwa mvuto
Mmoja wa waliohojiwa anasema “Nilikuwa na mpenzi wangu kwa muda wamiaka mitatu, alikuwa kijana mzuri sana na nilifurahia sana ninapokuwa naye lakini tatizo nikwamba hakukuwa na chembe ya mvuto baina yetu. Wengi wa marafiki zetu walikuwa wameshachumbiana na kuvishana pete lakini kila mchumba wangu alipojaribu kuanzisha hoja ya kunivisha pete nilijitahidi sana kubadilisha mazungumzo ili tu tusiklizungumzie hilo.
Ipo siku nilisafiri kikazi na huko nikakutana na na kijana mfanyakazi mwenzangu ambaye taratibu nilijikuta naanza kuvutiwa nae. Kwakweli ulikuwa wakati mzuri sana, labda kwasababu niliitarajia safari hii kwa muda na nilikuwa sijasafiri kwa muda pia na ukizingatia nimekutana na mtu ninaevutiwa nae basi mambo yalikuwa mazuri zaidi.
Wakati wa kurudi ulipofika nilirudi nyumbani nikatengana na mchumba wangu na kujikuta sasa naanza mahusiano rasmi na yule kijana niliyefanyanae kazi kule nilikoenda. Ingawa siwezi kusema najisifia kwa nilichokifanya, lakini namshukuru Mungu kwamba mambo yaliendelea kuwa mazuri upande wangu kwa sababu mimi na yule kijana tuliamua kuoana na hadi sasa tunaishi kwa furaha na mapenzi mazuri”.
Kuchelewesha kitendo cha kuachana
“Kabla tu sijaenda kuachana na mwanaume aliyekuwa mpenzi wangu, niligundua kuwa alikuwa na hali mbaya sana kihisia, hakuwa tayari kabisa kusikia kwamba tunaachana nahii ikanifanya kukosa ujasiri wa kumtamkia kuwa tuachane. Kwahiyo nikasubiri kama mwezi mmoja hivi ili haliyake irudi kuwa njema ndiyo nimwambie.
Mara tu haliyake ilipokuwa sawa na wakati na mimi nimeshaanza kupata ujasiri wa kumwambia mara akafukuzwa kazi, nikajihisi tena nimerudi katika hatua ya kwanza. Wakati huo sasa tayari nilishakutana na kijana ambaye nilishatamani sana kuanza naye mahusiano, na kwa kushindwa kujizuia na kwahali niliyokuwa napitia kimahusiano nikajikuta nimemruhusu awe mpenzi wangu, pasipo hata kumhusisha mpenzi wangu wa awali kuwa sasa nipo katika mahusiano mengine.
Nahisi nilijipamoyo kwamba siwezi kumwambia sasahivi wakati hali yake yakihisia haikuwa nzuri”. (Binti aliyehojiwa hapa alikuwa na miaka 30, wakati yule wa kwanza alikuwa na miaka 33)
Madhara ya kuwa mbali na mpenzi wako
“Mimi na mchumba wangu tuliamua kuendelea na mapenzi yetu tukiwa mbalimbali mara tu nilipopata nafasi ya kwenda chuo kikuu mbali na nyumbani. Miezi michache ya kwanza haikuwa na shida, kila kitu kilikuwa sawa na tuliwasiliana bila shida.
Lakini kila muda ulipokuwa ukienda nikajikuta naanza kuvutiwa na kuwa karibu na kaka mmoja aliyekuwa mwanafunzi mwenzangu na mara kwa mara nilikutana naye maabara za sayansi. Baada ya masomo kumalizika nilirudi nyumbani na nilimkuta mchumba wangu akinisubiri kwa hamu sana. Kwakweli kukaanae kipindi hiki haikuwa rahisi kabisa ingawa sikuweza kuachana nae wakati huu sababu bado nilivutiwa nae.
Ziko nyakati hapa katikati nilimtembelea yule mwanafunzi mwenzangu niliyevutiwa nae tukiwa chuoni na nikagundua kuwa kilichokuwa baina ya mimi na yeye kilikuwa ni hisia zaidi nasio penzi haswa, ingawa tulishajikuta tukiingia katika penzi, nahisi hii yote ilisababishwa tu na upweke na kuwa mbali na mwenzangu, basi nikaamua kuacha kabisa kuwasiliana na yule mwanafunzi mwenzangu na kuweka mawazo yangu yote kwa mpenzi wangu kwasababu nilijua kuwa yeye ndio alikuwa wangu wa maisha, nasikitika kwamba sikuwahi kumwambia kilichoendelea wakati nikiwa chuoni, ingawa maranyingine najihisi kushtakiwa moyoni. Maranyingine najipa moyo kwamba ule ulikuwa utoto na ujinga tu. Sasa mimi nayeye tunaendelea vema na ni miaka mine sasa tangu nimemaliza chuo kikuu”.
Kuepukana na kuwa mpweke
Binti huyu mwenye miaka 28 anasema “Nilianza tu kuhusiana kimapenzi na kijana niliye naye sasahivi mara baada ya kuachwa na mpenzi niliyekuwa naye kwa miaka miwili.
Kwakweli ilikuwa ngumu sana kwangu na huyu mpenzi wa sasa kweli aliniokoa katika maumivu hayo, baada ya mimi nayeye kuwa katika mahusiano kwa miezi mitano hivi, mpenzi wangu wa kwanza akarudi na kuomba nimruhusu na kumpa nafasi tena na kuahidi kuwa hayatotokea tena. Ukweli ni kwamba bado nilihisi kumkosa sana moyoni mwangu, kwahiyo tukaanza kuonana mara kwa mara ingawa sio kwamba nilikuwa nimeachana na huyu niliyekuwa naye sasa.
Najihisi nilikuwa nimemuweka huyu kijana wa sasa karibu ili kujihakikishia usalama zaidi maana sikuwa nikijiamini sana kuwa na yule wa awali, nilihofia kama ataniacha tena angalau ninamtu pembeni yuko tayari kwa ajili yangu, ingawa sio kwamba nilimpenda kiukweli kama mpenzi wangu wa mwanzoni.
Kwa bahati mbaya mimi na mpenzi wangu wa awali hatukuweza kuendelea vema hata baada ya kumpa nafasi ya pili aliyoiomba, mbaya zaidi nikwamba mpenzi wangu wa sasa alipogundua kuwa nilikuwa ninaonana mara kwa mara na yule wa kwanza na yeye akasema hatoweza kuendelea na mimi. Kweli nilijifunza somo hapa kuhusu kuhusiana na wanaume wawili wakati mmoja, na pia kujifanya najaribu kulea nakubembeleza penzi lililokwisha kufa”.
Kutafuta pumziko baada ya mahusiano mabaya
“Nilipokuwa binti mdogo (sasa hivi nina 30) nilikuwa katika mahusiano na kijana mmoja ambaye kwakweli alikuwa akinipinga katika kila ninachokifanya, alinikejeli sana kuhusu maumbile yangu na uzito wangu, mara aseme mimi mjinga, mara sijui kitu, mara mi mshamba na mambo mengine mengi mabaya.
Pamoja na mabaya yote haya bado niliamua kuwa naye tu ingawa marafiki zangu wote na wazazi na ndugu zangu walimchukia. Siku moja nikiwa kwenye sherehe nikakutana na kijana mmoja na gafla tulijikuta tumezama kwenye maongezi ya mapenzi na hisia zetu kuvaana. Yani huyu alikuwa ni tofauti kabisa na mpenzi wangu, wametofautiana kilakitu kuanzia maneno hadi matendo, yani ni kijana mpole, mzuri wa tabia, mkarimu na ananitia moyo badala ya kunivunja moyo.
Mara kwa mara tulikuwa wote tukifurahia siku za mwisho wa wiki,na moyoni mwangu ikawa kama vile taa ya yule wa kwanza ndiyo imezima kabisa. Kwa mara ya kwanza nilimbusu usiku kabla hajaondoka kurudi nyumbani kwao, na nilipoenda kuonana na yule wa kwanza nilimwambia tuachane. Niliamua kuendelea sasa rasmi katika mapenzi na mpenzi wangu mpya na baada ya miaka mitatu tukaamua kuoana”.
Jitihada za kutafuta kile unachohisi kukikosa
“Mimi ni binti niliyekulia katika mikoa ya pwani kwahiyo napenda sana kwenda fukweni kukaa, kuogelea na kupunga upepo. Kwa bahati mbaya mpenzi wangu amekulia zaidi bara kwahiyo mambo ya fukweni kwake sio kitu kabisa na hapendi, mara kwa mara tumekuwa na ushindani na mikwaruzano kuhusu wapi twende tukapumzike na mara zote yeye ndio anashinda.
Baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa muda wa miezi nane, kuna wakati nilisafiri mimi na rafikizangu na tulitumia boti kwa muda mrefu wa safari, nahodha wa boti hii alikuwa kijana mzuri, mtanashati na anaonekana ni mtu wa maisha ya fukweni zaidi, kweli nilivutiwa nae, Tulipofika tuliahidiana kuonana usiku ule na tulikuwa na wakati mzuri sana pamoja, sikuwahi kumwambia mpenzi wangu kuhusu yaliyoendelea katika safari yangu, na wala sijihisi kushtakiwa moyoni mwangu, tena kuna maranyingine najihisi ndani yangu kuwa kile ndicho kilikuwa chema kumfanyia huyu mpenzi wangu kwasababu ya utukutu wake.
Bahati mbaya sana mimi na mpenzi wangu hatukuweza kuendelea sana, tuliachana baada ya mimi kushindwana naye na niliamua kuhakikisha kwamba kila kijana nitakayeamua kuhusiana naye basi lazima ayajue maisha ya fukweni”.
Jitihada za kumuadabisha (kumkomesha)
“Mpenzi wangu wa mwisho alikuwa na tabia za wanawake sana kabla hatujaamua kuanza neye mahusiano, nilidhani ningeweza kumbadilisha tabia yake hiyo lakini nilijidanganya, mara kwa mara nilisikia tetesi kuwa alikuwa anaonana na wasichana wengine wakati bado tuko naye katika mahusiano, lakini kila nilipomuuliza marazote alikataa katakata.
Usiku mmoja nilipata simu kutoka kwa msichana ambaye walikuwa wamehusiana naye kwa miezi mitatu na akaniambia kuhusu msichana mwingine pia ambaye na yeye amegundua kuwa anamahusiano na huyu mpenzi wangu. Nilikuwa na hasira sana usiku ule, niliamua kutoka na marafiki zangu nikiwa nimevalia mavazi ya kumvuta kila mwanaume ambaye aliniona, na nikaamua kuwa na muda na kijana fulani mzuri sana niliyekutana naye katika mtoko ule.
Ndani yangu nilipata kupumua kidogo nikajihisi kuwa angalau hicho ndiyo alichostahili mpenzi wangu huyu, nilitamani na nilifurahia kuuona uso wake jinsi anavyokuwa wakati nikimpa taarifa ya nilichokifanya usiku ule na ninayoyajua kuhusu yeye na wanawake zake na hatimaye nikamwambia kila mtu achumue muda wake, na tukaachana”.
No comments:
Post a Comment