Saturday 25 November 2017

Lukuvi awataka walionunua viwanja wakadai fedha zao Halmashauri


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amefuta viwanja vilivyokuwa vimepimwa katika  eneo la Mawelewele pamoja na mchoro wake kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu.

Lukuvi amewataka  watu wote walionunua viwanja katika eneo hilo waende ofisi za Halmashauri ya Manispaa kudai fedha zao.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea wa CCM kupitia Chama hicho  Baraka Kimata  kwenye kata ya Kwiru.

 Lukuvi amesema  amefikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali na pia kufanya uchunguzi wake binafsi.

 “Nimefuta mchoro  wa upangaji eneo lile na ule wa upimaji yote nimefuta leo(jana) na nimeagiza watu waliouziwa eneo lile waende wakadai fedha zao halmashauri iwarudishie” amesema Lukuvi na kuongeza

“Haiwezekani leo hatuna vyumba vya madarasa vya kutosheleza halafu unachukua eneo kubwa kama lile unaligawa kwa watu wachache” amesema

Katika hatua nyingine Lukuvi aliwataka wakazi wa Kitwiru kuchagua Kimata na kwamba mara atakapoichaguliwa yeye atafika katika kata hiyo kusikiliza kero za ardhi.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa hiyo Alex Kimbe amesema  uamuzi huo ni wa kisiasa na umelenga kurudisha nyuma maendeleo katika halmashauri hiyo.

Amesema  eneo hilo ni  mtu binafsi ambaye ni Japan Kiluka  ambaye alilitoa  kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Msingi Mawelewele.

Amesema  mmiliki alikuwa na malalamiko yake ya muda mrefu Alisema mmiliki huyo aliomba katika viwanja vilivyopimwa apewe viwanja 18 na vinavyobaki iwe mali ya halmashauri jambo ambalo walilitekeleza.

 “Niwatoe hofu wananchi wa Iringa ,wale wote walionunua viwanja tutajipanga tutawarejeshea fidia zenu, lakini nisisitize kuwa uamuzi huo utaigharimu  Manispaa zaidi ya Sh 40 milioni kwani kila kiwanja kiliuzwa kwa Sh 5 milioni” amesema

Naye  Diwani wa kata ya Mshindo Ibrahimu Ngwada amesema hatua ya upimaji wa viwanja hivyo ililenga kuwanufaisha watu wachache na kwamba yeye alikuwa analishitaki suala hilo kwa waziri.

 Mwananchi.


No comments:

Post a Comment