MSHAMBULIAJI Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe anatarajiwa kurejea leo timu yake, Yanga ikimenyana na Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Tambwe hajacheza mechi hata moja ya mashindano msimu huu, baada ya kuumia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Chipukizi Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba Agosti 20 mwaka huu, Yanga ikijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Simba.
Na baada ya kufanya mazoezi mfululizo wiki hii, ikiwa ni mara ya kwanza kufuatia kushindwa kufanya mazoezi japo kwa siku mbili mfululizo awali, kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina anatarajiwa kumtumia Tambwe katika sehemu ya mchezo wa leo.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dissmas Ten alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba Tambwe yuko fiti na atakuwepo kwenye mchezo wa leo.
Ten alisema majeruhi ambao wataendelea kukosekana katika kikosi hicho ni Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma ambao wote wanapambana na hali zao warejee uwanjani mapema.
Kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi alikuwa anasumbuliwa na Malaria naye anaweza kukosekana katika mchezo wa pili mfululizo leo, baada ya kutokuwepo pia wakati Yanga ikiichapa 5-0 Mbeya City Jumapili iliyopita.
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliendelea jana kwa mchezo mmoja tu, wenyeji Ndanda FC wakilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Njombe Mji FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mechi nyingine za leo, Singida United watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Namfua, Singida, Mbao FC wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagera Sugar wataikaribisha Stand United Uwanja wa kambarage Shinyanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Maji Maji Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Kesho Simba SC watakuwa wenyeji wa Lipuli ya Iringa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV utakamilishwa Jumatatu ijayo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji, Azam FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment