Saturday 25 November 2017

Kocha K'Njaro Stars kuwapeleka wachezaji Ulaya




Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania bara Kilimanjaro Stars Ammy Ninje, amesema yupo tayari kuwasaidia wachezaji wa Tanzania kwenda kucheza soka barani Ulaya.

Ammy Ninje ambaye ataiongoza timu hiyo kwenye michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya mapema mwezi ujao amesema yeye yupo tayari kutumia uzoefu wake barani Ulaya kuwatafutia timu wachezaji watakaoonesha viwango.

“Mimi nina ‘Network’ ya walimu wenzangu kwenye nchi za Ulaya kama Sweden, hivyo nitawasaidia wachezaji wenye vipaji vya kucheza Ulaya kuweza kupata vilabu ili wakacheze soka la kulipwa, na kama nchi tuwe na ‘professional’ wengi”, amesema Ammy Ninje.

Kocha huyo ameyasema hayo kwenye mahojiano na kipindi cha Hotmix  jioni ya leo Novemba 24, ambapo amesema yupo tayari kutumia uzoefu wake wote ili nchi ifanikiwe na kufikia viwango vya mataifa kama Uganda na zaidi ya hapo.

Kuhusu michuano ya Challenge Ninje, amesema atajipanga vyema na kikosi cha wachezaji 20 ambao aliwataja hivi karibuni kwaajili ya michuano hiyo na anaamini wakishirikiana vyema wataibuka mabingwa.

Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Desemba 3 na kumalizika Desemba 17 nchini Kenya ambapo Tanzania ipo kundi moja na timu za Zanzibar Heroes, Rwanda, Libya na wenyeji Kenya. Kilimanjaro Stars itacheza mchezo wa ufunguzi Desemba 3 dhidi ya Libya.

No comments:

Post a Comment