Friday, 24 November 2017

Kinana, Nape waunganisha nguvu tena



     Arumeru. Katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mbunge wa Mtama, Nape Nnauye wameunganisha nguvu katika Kata ya Makiba ambako wanampigia debe mgombea wa chama hicho, Samson Laizer.

Kinana na Nape wanachukuliwa kama wanasiasa waliofanya kazi kubwa ya kuhuisha nguvu ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita baada ya kuzunguka karibu nchi nzima kupiga siasa na wakati mwingine kudiriki hata kuwasema hadharani mawaziri wa Serikali ya CCM, wakiwaita mizigo.

Jana wawili hao waliungana na Mrisho Gambo, ambaye ni mkuu wa mkoa wa Arusha na Alexander Mnyeti (Manyara) kuipigia debe CCM.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Makiba wilayani Arumeru, Kinana alisema ni vigumu vyama vya upinzani kushika nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Kinana alisema akiwa katibu mkuu wa CCM ametembelea mikoa, wilaya na kata tofauti ambako ameona wananchi wana imani kubwa na chama hicho.

Kinana alisema katika uchaguzi mkuu uliopita wananchi wa eneo hilo walipiga kura kwa kufuata upepo na ushabiki wakidhani upinzani ungeshinda.

“Watu walidhani rafiki yangu yule, mnamjua siwezi kumtaja, atakuwa Rais, lakini hakuweza kupata nafasi hiyo,” alisema Kinana.

Alimpongeza Gambo kwa kufanikisha maendeleo ya mkoa huo na hasa eneo la Makiba.

“Pia mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alifanya kazi kubwa alipokuwa mkuu wa wilaya ya Arumeru. Anastahili hongera nyingi,” alisema Kinana.

Alisema maendeleo hayana ushabiki hivyo wananchi wa Makiba wanapaswa kumchagua Laizer ili asimamie maendeleo.

Alisema miradi ya maendeleo kama wa umeme vijijini (Rea), maji, ujenzi wa barabara ya Mirerani unapaswa kusimamiwa na diwani wa CCM na si wa upinzani.

Alisema CCM ndicho chama kilichoshinda uchaguzi hivyo kinatekeleza ilani yake na hata wapinzani wanatekeleza ilani hiyo.

Naye Nape, ambaye alizunguka nchini na Kinana wakati akiwa katibu wa itikadi na uenezi, alisema wananchi wa kata hiyo wasirudie makosa kwa kuweka ushabiki na kumchagua mgombea wa upinzani.

Alisema kata hiyo ni ya CCM ndiyo sababu wanaitaka kwa gharama yoyote kiasi cha viongozi kwenda eneo hilo kushiriki katika kampeni. Aliwataja viongozi hao kuwa ni yeye mwenyewe, Kinana na wakuu wa mikoa ya Arusha na Manyara.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer alisema ameshapeleka ombi la wananchi wa mkoa huo kuwa walikosea kwa kuchagua upinzani mwaka 2015.

Laizer alisema salamu hizo ameshazifikisha na Rais Magufuli ameridhia kutoa msamaha kwa wananchi wa eneo hilo ambalo walidhani kanda ya kaskazini inatosha kumchagua Rais wa nchi.

Mgombea Laizer aliwaomba wananchi wa kata ya Makiba kumchagua kwa wingi awe diwani wao kwa ajili ya kusimamia maendeleo ya eneo hilo.

Laizer aliwaahidi utumishi uliotukuka pindi wakimchagua kwani yeye ni mtu wa maendeleo na anayeweza kutumwa kwenye halmashauri ya wilaya ya Meru.

Naye Mnyeti, ambaye ametajwa katika kashfa ya tuhuma za kuhonga madiwani wajiondoe CCM na hivyo kusababisha uchaguzi mdogo unaoendelea sehemu mbalimbali nchini ukiwemo wa kata hiyo, alisema wananchi wa eneo hilo walishamuahidi kuwa watamchagua mgombea wa CCM hivyo hana wasiwasi na hilo.

Mnyeti alisema kwa muda wote aliokuwa mkuu wa wilaya hiyo alishirikiana na wananchi wa Makiba, hivyo watamchagua mgombea wa CCM ili ashirikiane ipasavyo na mkuu mwingine wa wilaya hiyo atakayechaguliwa na Rais.

Naye Gambo alisema wananchi wa kata hiyo wanapaswa kumchagua mgombea wa CCM ili ashirikiane naye kuleta maendeleo.

Gambo alisema awali walifanya makosa kwa kumchagua mpinzani hivyo wasifanye tena makosa.

No comments:

Post a Comment