Jackson Makundi, baba mzazi wa mwanafunzi aliyeuawa wa Shule ya Scholastica, amemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati tukio la kifo cha mwanaye ili haki itendeke.
“Ninamuomba Rais ambaye ni wa wanyonge alisimamie suala hili ili haki itendeke. Nina uchungu na mwanangu kuuawa kikatili na kuzikwa bila kusitiriwa,” alisema jana wakati yeye na wanafamilia wenzake wakizungumza na waandishi wa habari.
Alisema wanashangazwa ni sababu za Wizara ya Elimu kutosema lolote kuhusu tukio la kuuawa kwa mwanaye Humphrey.
“Ninaamini Rais wangu tunayempenda na mtetezi wa wanyonge atatenda haki na ukweli wa tukio hili na waliolitenda wajulikane,” alisema Makundi. Pia, aliziomba taasisi zinazojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu kuingilia kati suala hilo alilosema ni la kijamii na linatakiwa kuchukuliwa hatua kali kwa kuwa kukaa kimya kunaweza kuendelea na kumtokea kwa mzazi mwingine.
Wakati huohuo, mmiliki wa Shule ya Scolastica iliyopo Himo, Edward Shayo amesema hahusiki kwa namna yoyote na kifo cha mwanafunzi huyo aliyekuwa kidato cha pili.
Alisema iwapo anajua chochote, basi damu yake isibakie duniani na kwamba anaumizwa na maneno ya uongo dhidi yake.
Wakati akisema hayo, taarifa zinadai mmoja wa walinzi wa shule hiyo ametoa maelezo polisi akikiri kumpiga na kusababisha kifo cha mwanafunzi huyo. Hata hivyo, kamanda wa polisi wa mkoa, Hamis Issah amekuwa hazungumzii suala hilo kila anapoulizwa kwa madai kuwa waandishi wanaingilia upelelezi.
Akizungumza na gazeti hili akiwa wodi namba 16 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC alikolazwa, Shayo alisema walifanya kila lililo ndani ya uwezo wao kumtafuta mtoto huyo.
Awali Kamanda Issah alisema mtoto huyo alitoweka shuleni Novemba 6. Hata hivyo, uongozi wa shule unadai alitoweka asubuhi ya Novemba 7 na mwili wake uliokotwa Mto Ghona Novemba 10 na kuzikwa Novemba 12 na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kabla ya kufukuliwa kwa amri ya Mahakama.
Shayo alisema baada ya kupokea taarifa za kutoweka kwa mtoto huyo, walimjulisha mzazi wake Jackson Makundi na baadaye taarifa zilitolewa Kituo cha Polisi Himo.
Kuhusu madai kuwa mmoja wa walinzi wake amekiri kumpiga mtoto huyo wakati akitaka kumrejesha shuleni baada ya kuruka ukuta, alisema haelewi mlinzi huyo ametoa wapi hadithi hiyo aliyoitaja kuwa ya uongo.
“Namuachia Mungu. Kuna maneno mengi yanaongewa lakini ukweli siku zote haufichiki na kama kweli mimi Shayo ninajua lolote kuhusu hiki kilichotokea, basi damu yangu isibaki duniani,” alisema.
Katika hatua nyingine, daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi aliyeuchunguza mwili wa mtoto huyo na kushauri uzikwe, anahojiwa na Polisi.
Habari za uhakika zinaeleza kuwa daktari huyo alikamatwa Novemba 19 baada ya uchunguzi mpya wa mwili huo kubaini haukuwa wa mtu mzima kama ilivyoelezwa awali na kwamba hakufa maji kama alivyoandika awali.
Gazeti hili lilimshuhudia daktari huyo akivalishwa pingu nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha KCMC, kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo za sababu ya kifo na umri wa mwili aliouchunguza Novemba 12.
Habari zinadai taarifa za daktari huyo na polisi wa Himo kuwa mwili uliookotwa ulikuwa wa mtu aliyekufa maji mwenye umri kuanzia miaka 35 na umeharibika, ndiyo zilichangia mwanafunzi huyo asitambuliwe.
No comments:
Post a Comment