Jokate Mwegelo ‘Kidoti’.
Rais John Magufuli.
Musa alipitia vitu vingi ikiwemo kejeli, kujaribiwa na hatimae kufanikiwa kuwavusha Wana wa Israeli kuelekea nchi ya ahadi. Lakini kuna wakati wafuasi wake hao walipojaribiwa kidogo tu wakaanza kunung’unika na kumkebehi Musa kwamba ni kheri maisha waliyokuwa wanaishi Misri kwa Farao.
Rais John Pombe Magufuli ameianza safari yake nyingine baada ya Novemba 5 mwaka huu kufikisha miaka miwili madarakani. Napenda kuifananisha safari yake hiyo iliyosheheni mageuzi makubwa sawa na ile ya Wana wa Israeli walipokombolewa na Nabii Musa kutoka kwenye mikono ya utumwa chini ya Farao wa Misri.
Uwajibikaji, Uzalendo, Utendaji
Kumekuwa na tatizo tatizo la watumishi wa Serikali kutokuheshimu misingi ya kazi zao katika utumishi wao wa umma, nidhamu ya kazi ilikuwa haipo. Ilifikia wakati watu walitunga safari za nje ilimradi tu wapate posho za kujiendeleza wao na familia zao.
Uzalendo wa nchi ukageuka kuwa uzalendo unaokimu mtu na familia yake na watu wake wa karibu. Fedha nyingi zikawa zinapotea angani na hata matunda ya safari tulikuwa hatuyaoni. Bado barabara na miundimbinu muhimu ilikuwa kasi yake ya kuimarishwa haikuwa nzuri sana.
Utendaji na ubunifu ulikuwa wa chini kwani hakukuwa na kitu kipya katika utendaji wa kazi kwa wengi zaidi ya kujitajirisha kupitia kodi za wananchi bila sababu zozote zile za msingi.
Manung’uniko yalikuwa mengi juu ya rasilimali za taifa. Kulikuwa na makundi mengi yakizungumza kwa lawama namna rasilimali zilikuwa zinatumika vibaya. Makundi haya yakihusisha Wanasiasa, Wasomi na hata baadhi ya Wananchi wenye kufuatilia maslahi na rasilimali za taifa. Nchi yetu pendwa ya Tanzania ‘kuibiwa’ umekuwa ni mjadala wa muda mrefu bila utatuzi au hatua yoyote kuchukulliwa.
Kuna wakati, nikiamini kwa nia njema na uchungu wa nchi yao na si siasa, baadhi ya wanasiasa walipaza sauti kusema kuwa ni aibu kubwa kwa nchi yetu kushindwa hata kumiliki ndege yetu. Walihoji: “Tutatangazaje utalii bila ya kuwa na ndege yetu?” Kwa ufupi kila kitu kilikuwa kikionekana kwenda sivyo. Na hapa sijagusia issue ya “mafisadi”
Kuingia kwa Magufuli madarakani miaka miwili iliyopita, ukiyatazama maisha yake, utakubaliana nami kuwa huyu ni kiongozi anayeishi na kujituma kwa ajili ya maslahi ya wananchi.
Hii inanikumbusha nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka kadhaa ya nyuma, niliwahi kumuona Rais wetu ambaye kipindi kile alikuwa ni Waziri akila sehemu mmoja wanafunzi katika kijiwe maarufu cha misosi kiitwacho “Harvard”.
Pale chakula ni cha bei ya chini kabisa, mlo kamili mzuri ulikuwa hauzidi elfu 1000. Ilikuwa ni sehemu ya sisi wanafunzi wa kawaida kula kwa sababu ya bajeti zetu ndogo. Kumuona yeye kama waziri pale kulipelekea mimi kuanza kuelewa Dkt. Magufuli ni mtu wa aina gani. Ni wazi kwamba ni mtu wa watu, hana makuu, hajikwezi na anapenda “ku-budget.”
Mageuzi na Mabadiliko
Sishangai miaka miwili tu ya uongozi wake akiwa ameacha tayari alama na mageuzi makubwa ya kukumbukwa. Kwa kifupi tu ametenda yafuatayo ya kukumbukwa:
· Kuwezesha elimu bure kuanzia shule ya Msingi hadi Sekondari;
· Kufufua shirika la ndege la ATCL kwa nunua ndege mpya sita;
· Kuongeza mapato ya ndani toka trilioni 9.9 kwa mwaka hadi trilioni 14 kwa mwaka;
· Kurejesha nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma;
· Ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania
· Kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma;
· Kutimiza ahadi ya Serikali kuhamia Dodoma;
· Kukamilisha miradi mikubwa wa umeme wa Kinyerezi I-extension na Kinyerezi II;
· Kuanza ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge;
· Uzalendo kusimamia raasilimali za taifa yakiwemo madini;
· Kuanza ujenzi wa barabara za juu Tazara, Ubungo na daraja la wapiti kwa miguu Furahisha;
· Ujenzi wa madaraja ya kisasa mfano la daraja la Kilombero;
· Kusimamia uhakika wa madawati maabara na maktaba katika shule zote nchini;
· Ujenzi wa maduka ya kisasa ya dawa za ndani ya kila hospitali ya Serikali;
· Kupambana vikali dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya nchini;
· Kutoa bima za afya za matibabu ya bure kwa wazee
· Kuhakikisha wanafunzi wanaostahili kupata mikopo ya elimu ya juu wanapatiwa
· Kuhakikisha Tanzania inakuwa na viwanda vya kutosha nchini
· Kufuta kodi na urasimu kwenye kilimo na uwekezaji nchini
· Kuhakikisha serikali inasimamia uuzwaji wa mazao ya wakulima masokoni na kupata faida. Mfano wakulima walikuwa wakiuza korosho zao kwa tsh 800 kwa kilo mpaka tsh 4000 kwak kilo.
Nimesukumwa kuzungumzia na kuorodhesha mafanikio haya kwa ufupi ili tujue shabaha ya rais wetu. Rais wetu anataka kurudhisha heshima. Heshima hailetwi kwa blah blah, heshima huletwa kwa vitendo na kufanya vitu kwa njia ya kuwa “disruptive”-kutokufanya vitu kikawaida au kwa mazoea.
Msimamo mkali wa rais
Rais Magufuli anataka kuona watu wakijituma na kuleta matokeo chanya. Hata ukiangalia safu zake za uongozi ni viongozi walioshiba kwenye nafasi zao. Na wanaonekana hawafai wanaondolewa. Ila bado kuna makundi ya watu kwenye jamii wanaona anachofanya ni kazi bure na kufikia hatua ya kuaminisha umma kuwa Serikali hii ya Awamu ya Tano imefanya hali imekuwa ngumu na eti haina malengo na kuwa imepoteza dira.
Hakuna ukombozi uliofanyika bila kutoa jasho, kutokwa damu na kutumia mbinu za kujifunga mikanda. Mheshimiwa Rais anafanya hilo, ni lazima kujitoa mhanga kwa kipindi hiki kwa ajili ya mafanikio ya muda mrefu. Nilifikiria viongozi wetu hasa wa upinzani wangefurahia mabadiliko haya kwa maana ndio kitu hasa walichokuwa wakikitamani na wakishiriki kikamilifu katika kutoa mawazo yenye kujenga ila hali imekuwa ni tofauti.
Hapa ndio maana nimekikumba kisa cha safari ya Mussa-maana nalifananisha hili na kadhia ya wale Wana wa Israeli kufikia hatua mpaka kumkufuru Mwenyezi Mungu na wakaona kuwa ni kheri wangebaki kule Misri. Kama kumbukumbu ya kuku, nao walisahau walipotoka.
Ushauri
Natambua ni vigumu kumuaminisha kila mtu ukweli kama tayari anaamini uongo, kama ilivyo vigumu kumuaminisha uongo yule ambaye anaamini ukweli. Ila kama vijana na taifa lililo la vijana, imefika wakati wa kila mmoja kusimamia kila anachokiamini, LAKINI asiamini kile alichoaminishwa. Vijana tuache siasa za kupikwa na kuungaunga, tusimame katika ukweli na mambo yale ambayo yana maslahi kwa taifa letu na si maslahi binafsi. Tujiulize: Inakuwa vipi, wanasiasa na wanaharakati wale wale ambao walikuwa wanapigania vitu flani vifanyiwe kazi, sasa vinafanyiwa ndiyo wa kwanza kununa na kufanya ‘confusion’ mbele ya Jamii?
Ndani ya chama cha Mapinduzi tunaamini Umoja ni Ushindi. Huu ni wakati wa kuungana na Mheshimiwa Rais katika ukombozi wa Watanzania, lazima tuelewe shabaha ya Rais wetu kuwa ana nia njema na maendeleo ya nchi yetu.
Hii safari sio rahisi, hakuna aliyemkamilifu ila wote tunaitumainia Tanzania yenye neema. Vijana tuache kupokea mapokeo ya wanasiasa wasio na nia njema na nchi yetu, tufanye kazi kwa kushirikiana katika kuiletea nchi hii neema.
Hapa Kazi Tu!
Jokate Mwegelo
Kaimu Katibu Idara Ya Uhamasishaji,
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) makao makuu
No comments:
Post a Comment