Saturday, 25 November 2017

Chadema yawaomba wapiga kura kukaa mita 100



Dar es Salaam. Chadema wamewataka   wapiga kura kukaa umbali wa mita 100  wakati wa kusubiri matokeo yao kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyia kesho katika kata 42 nchini, ili kulinda kura zao.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Jeshi la Polisi lilipinga wapiga kura kukaa umbali wa mita 100 na baadaye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuhitimisha sakata hilo kwa kutamka kuwa kukaa umbali wa mita 200, baada ya kupiga kura hairuhusiwi.

Akielezea mwenendo wa uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema,  Benson Kigaila amesema  sheria inaruhusu wapiga kura kukaa umbali huo ili kulinda kura zao.

“Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 inataka wapiga kura kusimama umbali wa mita 100, kwa hiyo tuwaambie wapiga kura wetu wakishamaliza kupiga kura wakae umbali wa mita hizo, waongeze na nyingine moja walinde kura zao,” amesema

Kigaila amewataka  wapiga kura hao kwenda kwenye vituo vya kupigia kura na kutimiza wajibu wao bila kuogopa kitisho chochote na baadaye walinde kura zao hadi zitakapotangazwa.

“Waende wakapige kura wasiogope kitisho chochote,” amesema a kuwataka baadaye waende kwenye makao makuu ya kata yatakako tangazwa matokeo hayo kuhakikisha, washindi wanatangazwa kwa haki.

Kiongozi huyo wa Chadema amesema kumekuwa matukio ya uvunjaji wa haki kwenye mikutano yao ya kampeni ikiwamo makada wake kuvamiwa na kupigwa.

“Upinzani ukishinda utatangazwa wapende wasipende, ambaye atatangaza matokeo tofauti ashughulikiwe kama mwizi mwingine wa kawaida kwa sababu wezi huwa wanashughulikiwa,”

“Kwa hiyo watu waende walinde haki yao ya kikatiba, wapige kura na walinde matokeo. Yatangazwe matokeo sahihi.” amesema  kiongozi huyo wa  Chadema

No comments:

Post a Comment