Friday 24 November 2017

Mastaa kibao kupamba kilele cha Fiesta kesho



MSIMU wa shamrashamra za muziki na kitamaduni katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wa Tigo Fiesta 2017, ulio na kauli mbiu ya ‘Tumekusoma’, unatarajiwa kuhitimishwa kesho kwenye viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam, ukihusisha wasanii zaidi ya 18.

Akizungumza tamasha hilo Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, alisema kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 16 ya tamasha hilo, Tigo Fiesta ilikuwa imewashirikisha wasanii wa Kitanzania pekee.

“Kilele cha msimu wa Fiesta 2017 kitawahusisha wasanii wa Kitanzania pekee. Tigo imejikita kuleta mageuzi makubwa kwa kuinua vipaji vya wasanii wa Kitanzania kama njia mojawapo ya kukuza sanaa na ajira kwa vijana nchini. Tumewakutanisha wasanii wetu maarufu na mashabiki wao katika mikoa yote 17 tuliotembelea na kuwajengea uwezo wa kutumbuiza laivu mbele ya halaiki kubwa ya watu,” alisema Mpinga.

Alisema kuwa, kupitia Fiesta 2017, wameibua vipaji vya muziki katika mikoa mbalimbali kupitia shindano la kuimba la Supa Nyota, ambapo washindi watapata fursa ya kutumbuiza katika kilele cha msimu kesho.

“Kununua tiketi ni rahisi. Fuata utaratibu wa kawaida wa kutuma pesa na tuma Sh 9,000 kwenda namba ya TigoPesa 0678 888 888. Hapo hapo utapokea ujumbe mfupi wa SMS unaothibitisha manunuzi yako ya tiketi. Hifadhi huo ujumbe mfupi. Baadaye utapokea maelekezo ya jinsi na wapi pa kwenda kuchukua tiketi yako. Bei halisi ya tiketi getini ni Sh 10,000,” alisema Mpinga.

Mratibu Mkuu wa Kamati ya Maandilizi ya Fiesta 2017, Sebastian Maganga, aliwataja wasanii watakaotoa burudani kesho katika tamasha hilo kuwa ni Ali Kiba, Aslay, Ben Pol, Barnaba, Chege, Darasa, Dogo Janja, Jux, Fid-Q, Rostam (Roma na Stamina), Rich Mavoko na Nandy.

Wengine ni Mr Blue, Vanessa Mdee, Maua Sama, Zaiid, Lulu Diva, Mimi Mars, Rosa Ree, Chin Beez, Nyandu Tozi, Nedy Music, Ommy Dimpoz, Bright, Weusi (Joh Makini, G-Nako na Nikki wa Pili) na wengineo.

Alisema kuwa, tamasha hilo kwa mwaka huu limezunguka katika mikoa ya Arusha, Kahama, Musoma, Mwanza, Tabora, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Kigoma, Morogoro, Tanga, Mbeya, Moshi na Mtwara.

No comments:

Post a Comment