Saturday 25 November 2017

Zitto Kabwe asema kinachotakiwa ni mabadiliko ya maendeleo kabla ya 2020


 

Mtwara. Kiongozi wa Chama wa ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kitendo cha kuchukua watu kutoka vyama vya upinzani siyo mafanikio bali kinachotakiwa ni kuwaletea wananchi mabadiliko ya maendeleo kabla ya mwaka 2020.

Zitto alisema hayo juzi katika mkutano wa kampeni za udiwani Kata ya Reli mjini Mtwara.

“CCM kazi yao sasa hivi ni kuchukua watu kutoka vyama vya upinzani, wanaona ni mafanikio wakisajili dirisha dogo. Huu mtaa wenu si ulikuwa hivi tangu mwaka 2015 kuna mabadiliko yoyote?

“Itakapofika mwaka 2020 mtaangalia wamechukua watu wangapi kutoka upinzani au mtaangalia mabadiliko kwenye mtaa wenu?” Alihoji Zitto.

Pia, alisema ameshangaa kuona foleni ya watu waliojipanga kwenye meli ya Wachina inayotoa huduma za afya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata huduma akidai hiyo ni dalili ya kuonyesha kuna tatizo.

Aliendelea kusema kuwa maendeleo si idadi ya madaraja, bandari na barabara za juu zilizojengwa bali ni afya, elimu na uwezo wa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi.

Zitto alisema kwa sasa Tanzania inajenga reli lakini inachukua vyuma kutoka Uturuki ikiwa ni pamoja na kampuni ya kuponda kokoto kwa ajili ya ujenzi wa reli.

“Nchi ya aina gani, kuna haja gani ya huu uhuru ambao tunao mpaka sasa? CCM inaamini ninyi nyote mtawapa kura,” alisema.

Mgombea wa udiwani wa kata hiyo, Mwajuma Hassan alisema kwamba vipaumbele vyake ni kuhakikisha kila mkazi wa kata hiyo anajiajiri.

Pia, mgombea huyo aliahidi kusimamia huduma za kijamii kama afya, maji na elimu.

Mwananchi:

No comments:

Post a Comment