Dar es Salaam. Kauli ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali imeiibua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo imetangaza kuanza mchakato wa kufuatilia ulipaji wake wa kodi.
TRA imesema uamuzi huo unatokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwamo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za mamlaka hiyo.
Na kama utajiri wake unatokana na sadaka pekee, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere aliwaambia wanahabari jana kuwa hilo litakuwa jambo la kushtua.
Kanisa hilo kupitia kwa mtendaji kazi wake, Natus Mwita limesema litatoa ushirikiano kwa TRA japo hadi jana mchana lilikuwa halijapokea taarifa rasmi kuhusu kauli hiyo ya TRA.
Kauli ya TRA imetolewa siku tatu tangu kusambaa kwa picha za video zikimuonyesha Askofu Kakobe akiwa katika mahubiri kwenye kanisa lake lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam, akisema kiwango cha fedha alichonacho si tu ni zaidi ya kile cha Serikali, bali pia anaweza kuwakopesha fedha hata mawaziri.
“Mimi sihitaji hela nina hela kuliko Serikali, si unaona shughuli yenyewe hii, sio pesa hii,” alihoji akionyesha waumini waliohudhuria ibada hiyo ambao nao walisikika wakijibu, “ni pesa.”
Alisema, “Nimewaambia waandishi wa habari hakuna wa kunihonga wala kunipa hela yoyote hata waziri akiwa hana hela aje kwangu nitamkopesha. Lakini neno hili lazima litapelekwa vilevile lilivyo. Mtawala akifanya dhambi, atajulishwa dhambi yake, hapa umekengeuka, hapa si njia upasayo kuiendea, njia ya kuiendea ni hii.”
Kwa taarifa hiyo ya ukwasi wa Askofu Kakobe, Kamishna Kichere alisema mamlaka hiyo imeipokea kwa furaha na inataka kujiridhisha juu ya vyanzo vyake.
Alibainisha kuwa TRA inafahamu kuwa shughuli za kidini hazitozwi kodi lakini inataka kufahamu kama fedha hizo za Askofu Kakobe zinatokana na sadaka pekee au kuna shughuli nyingine za kiuchumi.
“Tumefuatilia hakuna kumbukumbu za Askofu Kakobe kulipa kodi, sasa tumeona tumfuate ili maofisa wetu wakajiridhishe kama fedha hizo anazozizungumzia zinatokana na sadaka,” alisema.
“Na kama hana shughuli zozote za kiuchumi ikiwa ina maana utajiri huo unatokana na sadaka ni jambo la kushtua kidogo lakini sisi tutaishia hapo.”
Alisema, katika taarifa za mamlaka hiyo wapo watu wengi wenye fedha nyingi na kumbukumbu zao za kodi zipo lakini Askofu Kakobe si miongoni mwao.
Alimwomba Askofu Kakobe kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TRA watakaomtembelea kwa ajili ya ukaguzi.
Alipoulizwa kwa nini uhakiki ufanyike sasa na si miaka ya nyuma, Kichere alisema ni baada ya kusikia kwamba ana fedha nyingi kuliko Serikali wakati anafahamika kuwa ni kiongozi wa taasisi ya dini.
Askofu Kakobe alitoa kauli hiyo siku moja baada ya viongozi wengine wa dini kutumia mkesha na ibada ya Sikukuu ya Krismasi kuhimiza amani, upendo, kukemea maovu, kushauri viongozi wa Serikali kukubali kushauriwa na kutominya uhuru wa watu kutoa maoni.
Wakati maoni ya viongozi hao wa dini akiwamo Askofu Kakobe yakigeuka kuwa mjadala, Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali mstaafu Projest Rwegasira ilitoa taarifa ikiwataka viongozi hao kutojihusisha na masuala ya siasa, bali wajikite kuzungumzia mambo yanayoendana na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zao, vinginevyo zitafutwa.
Meja Jenerali Rwegasira alisema viongozi wa dini wanapaswa kujikita kuzungumzia masuala ya dini yanayoendana na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zao na kuachana na ya kisiasa.
Alisema ukiukwaji wowote wa sheria ni kosa linaloweza kusababisha jumuiya husika kufutiwa usajili kama ilivyoelezwa kwenye kifungu cha 17 cha sheria husika.
Hata hivyo, juzi katibu mkuu huyo alisema viongozi hao wa dini wakiisifia Serikali au viongozi wake hawatakuwa wametenda kosa lolote.
Mbali na kuzungumza katika ibada hizo, baadhi ya viongozi hao walitumia mitandao ya kijamii kueleza mambo yanayofanana na hayo.
Miongoni mwao ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza ambaye alitumia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook kuhoji mipaka ya kuzungumzia masuala ya dini na siasa, huku akitaka wananchi kutojengewa hofu ya kutoa maoni yao.
Jana alipoulizwa kuhusu ujumbe mwingine alioutuma katika mtandao huo alisema, “Kwa hiki kinachoendelea sasa, suluhu ni kufanyika kwa mjadala wa kitaifa ili kuwekana sawa.
“Anayezuia watu kuzungumzia siasa huyu anayezuia atakuwa hana historia vizuri, wakati wa Bunge la Katiba, kulikuwa na wawakilishi wa dini tena na wapiga ramli walikuwemo. Kama walitambuliwa na kushirikishwa katika kuandaa Katiba inakuwaje useme tusizungumze siasa, kama tuliingizwa Bunge la Katiba kwa nini sasa tunazuiwa kuzungumza,” alihoji.
Alisema, “Amri za kibabe au nguvu kwa viongozi wa dini sidhani kama zinajenga. Kuna viongozi wa dini wanaona wanajua siasa kuliko wanasiasa na kuna wanasiasa wanaona wanajua dini kuliko viongozi wa dini, ndiyo maana nikasema mjadala wa kitaifa unahitajika.”