MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kalambo na kamati yake ya ulinzi na usalama, kuandaa mkakati wa kumaliza uvuvi haramu katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Amesema uvuvi haramu unaoendelea katika mwambao huo, unahatarisha maendeleo ya viwanda vya samaki vilivyopo na hatimae kudhoofisha ajira za wananchi walioko karibu na viwanda hivyo, hivyo kukwamisha juhudi za serikali ya awamu ya tano katika maendeleo ya viwanda.
“Mwisho wa mwezi huu nataka taarifa ya namna mlivyojipanga kupiga marufuku uvuvi haramu ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na kuwakamata wale wanaokaidi na kuendesha uvuvi haramu. Vitendo hivi vikiendelea hiki kiwanda hakitakuwapo kwa sababu ya kuua samaki na watoto wake. Achaneni na uvuvi haramu, mnamaliza samaki katika ziwa letu hili,” alisema Wangabo alipokuwa katika ziara yake juzi.
Alisema samaki ndiyo rasilimali pekee inayowaajiri na kuendesha kiwanda na kuwataka wananchi kuungana kuhakikisha wanatunza na kupiga marufuku aina zote za uvuvi haramu. Pia alionya kuwa hataki kusikia kiwanda kimefungwa kutokana na kukosa samaki kwa sababu ya uvuvi haramu.
Katika ziara hiyo, Wangabo alitembelea viwanda viwili vya samaki vya Migebuka Fisheris Tanzania Limited na Akwa Fisheries Tanzania Limited, vilivyoko katika kata ya Kasanga. Kati ya hivyo, Migebuka ndicho kiwanda pekee kinachojikongoja huku Akwa kikiwa kimesimamisha uzalishaji.
Awali, akisoma taarifa ya kiwanda cha Migebuka, Mtendaji wa Kijiji cha Muzi, Gasper Kateka, alisema mbali na ukosefu wa samaki changamoto nyingine ni umeme na barabara jambo linalowafanya kutumia gharama kubwa kuendesha kiwanda hicho kwa majenereta na kupakia samaki kwenye boti hadi bandari ya Kasanga ili kuwasafirisha kwenda Sumbawanga kukwepa kipande cha barabara cha Km 1.2 kilichojaa mawe.
Kwa upande wake, Ofisa Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Godfrey Makoki, alisema makubaliano ya matumizi ya Ziwa Tanganyika yaliyofanywa na nchi nne (Zambia, Burundi, Tanzania na DR Congo) katika kikao kilichofanyika mwaka 2012 Bujumbura, Burundi, katika kanuni ya nne ya makubaliano hayo imekataza uvuvi wa dagaa mchana katika Ziwa Tanganyika.
“Jambo linalotupa shida ni uvuvi wa dagaa mchana. Kitaalamu dagaa huwa wanakuja kutaga mchana hivyo wanakuwa wakubwa kwa sababu wana mayai na usiku huwaoni, sasa huwa tunawaambia kuwa huo ni uvuvi haramu hapo inakuwa tatizo,” Makoki alibainisha.
Kuhusu changamoto ya umeme na barabara, Wangabo alimwagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Rukwa kuhakikisha umeme wa vijijini awamu ya tatu unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unawafika haraka katika kijiji hicho.
Pia alisema atawasiliana na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) na wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads) kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha ndani ya miezi mitatu wanairekebisha barabara ya Km 1.2 ili ipitike kwa urahisi.
Mwambao wa Ziwa Tanganyika kwa Mkoa wa Rukwa una viwanda vinne vya samaki. Viwili viko Kata ya Kipili Wilaya ya Nkasi na viwili vipo Kata ya Kasanga, wilaya ya Kalambo.