Hamad Ndikumana ‘Ndiku’ enzi za uhai wake.
DAR ES SALAAM: Wakati muigizaji nyota wa filamu nchini, Irene Uwoya akiwa nchini Rwanda kuhani msiba wa aliyekuwa mumewe, Hamad Ndikumana ‘Ndiku’, mama mzazi wa mwanasoka huyo wa zamani wa kimataifa, amewataja watu waliohusika kusababisha kifo cha mwanaye.
TUJIUNGE KWANZA NA UWOYA
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko kutoka Kigali aliko msibani, Uwoya alisema awali alipata taabu ya kufanya mawasiliano na ndugu na jamaa wa mumewe huyo wa zamani na baada ya kuwakosa, akaamua kuwasiliana na Asma, mwanamke ambaye siku chache nyuma, Ndikumana aliposti picha zake katika mtandao wa kijamii, akimnadi kama mpenzi wake.
“Nilipompata huyo, nikajitambulisha na kumwambia juu ya nia yangu ya kutaka kuja huku, katika namna ya kufurahisha, akanikubalia na tangu wakati huo ndiye nilikuwa nawasiliana naye na hata nilipofika hapa, yeye ndiye alinipokea na kunipeleka nyumbani kwa wazazi wa Ndikumana,” alisema muigizaji huyo. APELEKWA KWA
WAZAZI, WAMKUBALI
Uwoya ambaye alizaa na marehemu mtoto mmoja wa kiume aitwaye Krish, alisema baada ya kufikishwa nyumbani kwa wazazi wake, alipokelewa vizuri na ndugu na jamaa ambao walimweleza kuwa hawana kinyongo naye kwa sababu mambo yote yaliyotokea huko nyuma ni mapito ya duniani.
Irene Uwoya akiwa na Ndikumana enzi za uhai wake.
“Yaani huwezi kuamini, walinipokea vizuri sana, tofauti kabisa na huko nyumbani jinsi wanavyonizungumzia. Nimekaa nao na wao ndiyo walioniambia kitu ambacho kilinishangaza sana kuhusu chanzo cha kifo cha Ndikumana,” alisema Uwoya.
SIKU YA TATU MAMA MKWE AMDUWAZA
Uwoya alisema ilipofika siku ya tatu ya msiba, ambayo kwa kawaida ndiyo siku ya kuanua matanga, mama huyo alimweleza wazi juu ya watu ambao wanahusika na kifo cha mtoto wao, ambao familia inawatambua na inajua namna ya kushughulika nao.
“Mama Ndiku alisema anawafahamu waliomuua mtoto wao, alisema ni wachezaji wenzake sijui, wale watu wake wa mpira, wanasema chanzo ni kuwa yeye alikuwa mtu anayependwa na viongozi wa timu, hicho ndicho kilichowafanya wenzake wawe na wivu naye.
“Alinishtua sana, anasema wamegundua kuwa Ndiku aliwekewa sumu na wenzake na suala hilo linashughulikiwa na familia yao, sijajua watachukua hatua gani, lakini hicho ndicho kinachoendelea huku msibani,” alisema.
MANENO HAYO YAMEMFARIJI
Uwoya ambaye baadhi ya wadau wanamtaja kama mtu aliyesababisha msongo wa mawazo kwa mumewe baada ya hivi karibuni msanii Dogo Janja kung’ang’ania amefunga ndoa na muigizaji huyo, alisema kwa maneno hayo, amefarijika, kwani angalau mzigo wa lawama atautua.
“Maneno yalikuwa ni mengi sana kwa kweli huko nyumbani, kila mtu Uwoya Uwoya, afadhali mama amekata mzizi wa fitina, kifo chake wala siyo msongo wa mawazo, ni mchezo aliochezewa na wenzake huko kwenye mambo yao ya mpira,” alisema.
KWA NINI ALITAJWA UWOYA?
Kifo hicho cha ghafla cha Ndikumana, aliyefariki usiku wa Novemba 14 mwaka huu, kilisababisha baadhi ya watu kumtaja Uwoya kuwa huenda akawa chanzo kutokana na mtiririko wa matukio tangu ndoa ya wawili hao ilipovunjika miaka michache iliyopita.
Kwa muda wote ambao wawili hao walikuwa tofauti, Uwoya amekuwa akidai apewe talaka yake ili awe huru kuolewa na mtu mwingine, kitendo ambacho kinadaiwa kumuumiza mchezaji huyo wa zamani wa Stand United ya Shinyanga.
No comments:
Post a Comment