Friday, 24 November 2017

Lowasa asisitiza hana mpango wa kurudi CCM



WAZIRI Mkuu wa Zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameweka wazi tuhuma za madai ya kurejea Chama Cha Mapinudizi (CCM).

Juzi kupitia mitandao ya kijamii, kulikuwa na ujumbe wenye jina la Mrisho Gambo akidai amepokea ujumbe kutoka Monduli uliokuwa na ombi  kubwa moja.

Ujumbe huo uliokuwa umeandikwa kwenye ujumbe mfupi wa maneno, ulidai Mrisho ameombwa amuombee Mzee wa Monduli kwa Rais Magufuli ili akubali kumuona na yeye yupo tayari kurudi nyumbani kama rais atakubali kumuona.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya Makabi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, wakati wa kampeni za kumnadi mgombea udiwani, Lowassa aliibuka na kudai hana mpango wowote wa kurejea CCM kama ilivyodai mitandao ya kijamii.

Aliendelea kudai kwenye mkutano huo uliohudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo  hilo, Nasari Sumari, kwamba taarifa hizo zinazodai kuwa kuna watu amewatuma kuomba arejee CCM, si za kweli zimelenga kupotosha umma.

Lowassa ambaye amekuwa akizungumza kwenye maeneo tofauti kunadi wagombea wa udiwani Kanda ya Kaskazini, alisisitiza kwamba taarifa hizi zimejaa uongo wa kutunga.

“Watu hawa wamekuwa wakitunga mambo mengi juu yangu, naomba niwaambie Watanzania sina mpango wala ndoto za kurudi CCM,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo.

Lowassa aliyegombea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kufanikiwa kupata kura zaidi ya milioni sita, aliendelea kueleza kwamba watu hao wamekuwa pia wakisambaza uongo watu kuzuiliwa na Serikali kumtembelea nyumbani kwake.

“Yote haya ni maneno ya kutunga,” alisema Lowassa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli kabla ya kuhamia Chadema.

Kwa nyakati tofauti, Lowassa ameshiriki mikutano ya kampeni za kuwanadi wagombea udiwani katika Kata mbalimbali zilizopo mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Akiwa mkoani Arusha tayari amefanya mikutano katika Kata ya Moita Bwawani wilayani Monduli, Murrieti jijini Arusha, baadaye akaelekea mkoani Kilimanjaro akiwa huko msafara wake ulijikuta ukirushiwa mabomu ya machozi kwa lengo la kutawanya watu waliokuwa wamemzunguka.

Uchaguzi mdogo wa madiwani nchini unatarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu, baada ya madiwani waliokuwa wamepoteza sifa, huku wengine wakifariki na wengine kujiuzulu vyama vyao walivyokuwa wakivitumikia awali na hivyo kusababisha nafasi kuwa wazi.

No comments:

Post a Comment