Thursday 23 November 2017

Mgombea azuiwa kufanya kampeni



Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kufanyika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 nchini, mgombea wa Chadema wa Saranga amewekewa pingamizi la kufanya kampeni.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepanga uchaguzi mdogo wa udiwani kufanyika Novemba 26,2017.

Mgombea huyo, Ephraim Kinyafu wa Kata ya Saranga iliyopo Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam amewekewa pingamizi na Chama cha Wananchi (CUF) la kutofanya kampeni kwa siku zilizobaki.

Kampeni za uchaguzi huo zitahitimishwa Novemba 25,2017.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni mtendaji wa Kata ya Saranga, Dandasi Kijo amesema leo Alhamisi Novemba 23,2017 kuwa mgombea huyo amewekewa pingamizi baada ya kukiuka masharti ya kampeni.

Kijo amesema kanuni aliyokiuka ni kutamka akiwa jukwaani kuwa CUF haijasimamisha mgombea katika kata hiyo.

Akizungumzia pingamizi hilo, Kinyafu amesema hajashirikishwa kwa lolote hivyo hatambui uamuzi huo wa Jumanne Novemba 21,2017.

Kinyafu ambaye amekata rufaa ngazi ya wilaya, amesema katika kikao kilichofikia uamuzi huo Chadema iliwakilishwa na mjumbe badala ya katibu wa wilaya.

Mgombea huyo amesema hajawahi kupewa barua ya malalamiko wala muda wa kujitetea. Amesema rufaa aliyokata ngazi ya wilaya inasikilizwa leo.

No comments:

Post a Comment