Saturday 25 November 2017

Waziri Kigwangalla awajibu wanaosema vyuma vimekaza



Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Hamisi Kigwangalla amesema maisha yataendelea kuwa magumu kwa watu wasio na shughuli maalum ambao wamezoea kuishi kwa ujanja ujanja.

Ameyasema hayo wakai akijibu maswali ya wananchi kupitia mtandao wa ‘Twitter’ ambao wengi walitaka kujua kuhusu utendaji kazi wake na hali halisi ya maisha yalivyo wakidai kuwa ni magumu.

“Wanaofanya shughuli zao halali hawatoona vyuma vimekaza, badala yake watafurahia sema watoto wa mjini, wasanii sanii na wajanja wajanja ndiyo watapata shida! Hawa wajanja wajanja ni wangapi? Na wenye shughuli halali ni wangapi?”, alisema Kigwangalla akiacha maswali kwa mmoja wa watu waliomuuliza.

Waziri Kigwangalla aliendelea kwa kutoa ufafanuzi juu ya namna ya kujenga uchumi kupitia kufanya kazi na sio kutegemea kupata pesa kwa njia rahisi rahisi.

“Mfumo wa uchumi unataka watu tufanye kazi kwa ubunifu ndipo tupate maisha mazuri siyo kufanya usanii kidogo tayari ukatajirika! Kukaza vyuma maana yake kuziba mianya ya wasanii ili walio kwenye uchumi halisi na wasanii wawe sawa siyo kuonea watu!” alimaliza.

Waziri Kigwangalla hivi sasa yupo jimboni kwake Nzega vijijini akiwa amepiga kambi kwaajili ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Nata.

No comments:

Post a Comment