Tuesday, 21 November 2017

Jaji Warioba, Serukamba waumizwa kichwa na Mfumo wa elimu

Jaji Warioba, Serukamba waumizwa kichwa na Mfumo wa elimu



   Dar es Salaam. Waziri mkuu mstaafu, Joseph Warioba na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo na Huduma za Jamii, Peter Serukamba wamesema mfumo wa elimu unaotolewa sasa una kosoro hivyo unahitaji kufumuliwa na kuundwa upya.

Mbali ya Jaji Warioba na Serukamba, wadau wengine wamesema Tanzania ya viwanda haitafanikiwa ikiwa elimu itolewayo haiwaandai wahitimu kujitegemea badala yake wanakuwa tegemezi.

Hayo waliyasema jana katika kongamano litakalomalizika leo ambalo limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya HakiElimu linalojadili kuelekea Tanzania ya viwanda na Sera ya Ujamaa na Kujitegemea.

Jaji Warioba ambaye ni mwenyekiti wa kongamano hilo, alisema elimu inayotolewa inapaswa kuendana na mazingira ya wakati huu na kujibu mahitaji ya wahitimu.

Alisema licha ya mafanikio yanayofanywa na Serikali, kuna changamoto kubwa hususan ubora wa elimu inayotolewa kutowaandaa wahitimu kujitegemea kama ilivyokuwa awali.

“Uwiano wa wanafunzi wanaomaliza shule na wanaoendelea sekondari ni mdogo, wanaomaliza sekondari na kwenda chuo mdogo zaidi. Zamani mtu akimaliza darasa la nne anajua kusoma, kuandika na kuhesabu lakini sasa mtu anamaliza darasa la saba hajui kusoma, kuandika na kuhesabu,” alisema Warioba ambaye ni Jaji mstaafu na kuongeza: “Kuna matatizo makubwa ya miundombinu katika shule na vyuo kama madarasa na nyumba za walimu. Vitendea kazi na idadi ya walimu katika ngazi zao na maslahi ya walimu ni tatizo, haya yote yanatakiwa kupata majibu.”

Jaji Warioba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema: “Siku hizi watu wanamaliza lakini hawana la kufanya, lazima tujiulize elimu yetu ni bora kwa mazingira ya baadaye?

Naye Serukamba ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM) akichangia mada alisema: “Wote tunakubali tatizo lipo ila hatujui lini tunalimaliza. Umefika wakati tukae tuangalie mfumo, tuangazie elimu ya awali hadi vyuo vikuu.”

Alitaja maeneo yanayohitaji kuangaliwa kuwa ni ubora wa elimu inayotolewa, ufundishaji, uongozi, muda wa kusoma na maudhui kuanzia chini hadi juu.

“Tukifikia hapo tutaweza kujibu challenges (changamoto). Tunapaswa kuufumua mfumo wetu tuunde tume ya elimu ambayo itakuja na majibu ya wapi tuboreshe... leo wanaokwenda kusoma ualimu si waliofaulu vizuri, ukiangalia Finland anayekwenda kusoma kafaulu vizuri na mtumishi anayelipwa vizuri ni mwalimu,” alisema Serukamba.

Makamu mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala alisema elimu bora ni ile inayomfanya mtu aweze kutumia maarifa na ujuzi alioupata kupambana na mazingira yake.

“Elimu sahihi ni ile inayoondoa pengo kati ya maarifa ya kinadharia yanayotolewa darasani na yale ya vitendo yanayopatikana katika jamii. Elimu mwafaka ni elimu ya kujitegemea,” alisema.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, mkuruenzi mtendaji wa HakiElimu, John Kalage alisema: “Tunahitaji kuuangalia mfumo, je unajibu mahitaji ya sasa, je mfumo gani tuutumie sasa, kwani uliopo umeshindwa kuwaandaa wahitimu watakaokwenda kujitegemea na si kuwa tegemezi?”

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi (Tamisemi), Suleiman Jafo alisema Serikali itayachukua mapendekezo yote watakayofikia na kuyafanyia kazi.

“Tupo pamoja, Rais John Magufuli amefurahishwa na ninyi wasomi kukutana kujadili ikiwamo suala la uchumi wa viwanda na yeye amesema atakuwa tayari kupokea mapendekezo mtakayoyafikia na kuyafanyia kazi,” alisema Jafo.

“Taifa hili litajengwa na sisi wenyewe, tutumie kongamano hili kujadili kwa kina bila woga kwani tusipojenga msingi mzuri wa elimu yetu katika ushirikiano huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, tutakuwa wasindikizaji,” alisema.

Naye Waziri wa viwanda, Charles Mwijage alisema: “Hakuna hofu mtu kujitathmini wapi ametoka, yupo wapi na anakwenda wapi.”

Mwigage alisema tayari ameagiza uongozi wa Chuo cha Biashara (CBE) kutoa kozi kwa kila mwanafunzi ya ujasiriamali ili kuwawezesha wanapohitimu waweze kuwa wajasiriamali. 



No comments:

Post a Comment