Tuesday, 21 November 2017

Dk Kaunda kwenda kumshawishi Mugabe ajiuzulu


Harare, Zimbabwe. Chama tawala cha Zanu-PF kimewaita wabunge wake ili kuwapanga waanzishe mchakato wa kumshtaki bungeni Rais Robert Mugabe huku kukiwa na taarifa kwamba rais wa zamani wa Zaimbia, Kenneth Kaunda anakwenda kumshawishi mpigania uhuru mwenzake ajiuzulu.

Taarifa kutoka Lusaka, Zambia zinasema Rais Edgar Lungu amemtuma Dk Kaunda kwenda Harare kujaribu kumshawishi Rais Mugabe “ajiuzulu kwa heshima” baada ya jeshi kutwaa madaraka wiki iliyopita.

"Dk Kaunda alisafiri kwa ndege ya rais na ametua Harare," ofisa mwandamizi wa serikali ya Zambia aliliambia jana shirika la habari la Reuters. Kaunda ana umri wa miaka 93 sawa na Mugabe.

Hazijapatikana habari zaidi juu ya safari hiyo. Lakini ndani ya makao makuu ya Zanu PF, gazeti la NewsDay la Zimbabwe limripoti kwamba mbunge mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutoandikwa jina alisema kikao cha wabunge wa chama tawala kiliitishwa kujadili hatua ya kumshtaki mwanampinduzi huyo ambaye taifa linamtaka astaafu.

"Tumeitwa na tumeambiwa tufike kwenye makao makuu ya chama kabla au ifikapo saa 8:30 mchana leo (jana)” alisema. Mnadhimu mkuu wa Zanu-PF Lovemore Matuke alithibitisha habari hizo na kwamba kikao kilitarajiwa kuanza saa 10:00 jioni.

Chama cha Zanu PF, ambacho Mugabe alikiasisi na kukiongoza kwa miongo kadhaa Jumapili kilitoa tamko la kumfuta uongozi wa chama na kikamtaka awe amejiuzulu urais kufikia saa 6:00 mchana jana vinginevyo asubiri kushtakiwa na kuondolewa bungeni.

Mugabe alipuuza hali ambayo Rais Lungu ameamua kumtumza Dk Kaunda ili mkongwe huyo aliyetawala kwa miaka 37 tangu Zimbabwe ilipopata uhuru asiondolewe katika namna itakayomwondolea heshima.



Muda wa mwisho

Muda wa mwisho wa kujiuzulu kwa hiari ambao Rais Mugabe alikuwa amepewa na chama chake cha Zanu PF ulipita bila kutolewa taarifa rasmi huku uvumi ukienea kuhusu hatima yake

Japokuwa haijatolewa taarifa yoyote chanzo kilichokaribu na timu ya majadiliano upande mmoja wakiwemo majenerali waliotwaa madaraka wiki iliyopita kimeliambia shirika la utangazaji la CNN kwamba Rais Mugabe amekubali kung’atuka na kwamba ameshaandaa barua ya kujiuzulu.

Chanzo hicho kilidokeza kwamba majenerali wameridhia matakwa mengi ya Mugabe ikiwa ni pamoja na kupewa kinga ya kutoshtakiwa yeye na mkewe Grace, na abaki na mali zake.

CNN limeambiwa kwamba chini ya makubaliano hayo, Mugabe na Grace hawatashtakiwa. Pia, viongozi wawili waandamizi wa serikali ya Mugabe waliliambia shirika la habari la Reuters Jumapili kwamba Mugabe alikuwa amekubali kujiuzulu lakini hawakuwa wanajua yaliyomo katika mkataba wa kuondoka kwake.

Ili ionekane amejiuzulu rasmi, utaratibu ni kwamba barua lazima iandikwe kwenda kwa Spika wa Bunge, chanzo kingine kimeongeza.

Mugabe ambaye anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu kutoka kila kona aliwashangaza watu Jumapili alipokataa kufanya hivyo alipolihutubia taifa kwa njia ya televisheni akiwa ikulu.

Chama chake cha Zanu PF kimempa Mugabe, ambaye amekuwa katika kizuizi cha nyumbani na jeshi lililotwaa madaraka kimempa hadi mchana leo kuondoka vinginevyo atashtakiwa bungeni.

Jumamosi, maelfu ya Wazimbabwe walijimwaga mitaani kupaza sauti zao wakimtaka mzee huyo mwenye umri wa miaka 93, ajiuzulu.

Agoma

Jumapili mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 93 aliwashtua watu alipokataa wito wa kujiuzulu na hivyo kuitumbukiza Zimbabwe katika wiki ya pili ya mgogoro wa kisiasa huku juhudi za kuhitimisha utawala wake wa miaka 37 mfululizo zikikwama.

Chama cha Zanu PF alichoasisi na kukiongoza kwa miongo kadhaa kilitangaza kumwondoa kama kiongozi na kilimpa muda hadi Jumatatu mchana kuachia urais vinginevyo atashtakiwa bungeni.

Kabla ya kumwondoa Mugabe katika nafasi ya uongozi, Zanu PF ilitangaza kumrejesha katika chama makamu wa rais aliyefukuzwa Emmerson Mnangagwa kisha kikamteua kuwa kiongozi wake mpya. Mugabe alimfukuza Mnangawa Novemba 6 kwa madai ya usaliti hali iliyochochea mgogoro wa kisiasa.


No comments:

Post a Comment