Tuesday, 21 November 2017

Zelothe azungumza kimasai wakati akiomba kura




    Arumeru. Vituko na vioja vimezidi kutawala kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani Kata ya Musa mkoani hapa baada ya mgombea udiwani kupitia CCM, Flora Zelothe kuamua kuongea kimasai kwa lengo la kuwashawishi wananchi wampe kura.

Zelothe, aliamua kutumia lugha hiyo juzi wilayani Arumeru kama njia mojawapo ya kuwashawishi wapigakura wa eneo hilo ambao kwa asilimia kubwa ni makabila ya Wameru na Wamasai.

Akizungumza katika mkutano huo, Zelothe alisema wananchi wakimchagua atatekeleza mradi wa maji uliokuwa unagharamiwa na Benki ya Dunia eneo la Makutian ambao umesimama baada ya kuvurugwa na baadhi ya wanasiasa.

Akinadi sera zake kwa kimasai huku akiwa na mtafsiri wake pembeni aliwaambia wapigakura amejipanga kujenga shule ya sekondari.

Alisema kwa miaka mitano akiwa diwani wa viti maalumu alifanikiwa kuchonga barabara zote za vitongoji ndani ya Kata ya Musa kwa kiwango cha changarawe.

“Tutaboresha Shule ya Sekondari ya Kata ya Musa na kuleta walimu wa masomo ya sayansi na sanaa,” alisema Zelothe huku akishangiliwa.

Awali akimkaribisha jukwaani mwenyekiti wa CCM mkoani Arusha, Lekule Laiser alisema mgombea huyo ni mwanamke lakini ni jasiri na anajenga hoja.

Laiser alisema Zelothe aliwahi kwenda kupinga matokeo ya uchaguzi wa udiwani wa kata hiyo mwaka 2015 mahakamani na kusimamia kesi bila kuyumba na hilo linaonyesha dhahiri anafaa kuwa kiongozi.   

No comments:

Post a Comment