Sunday, 19 November 2017

Nyota ya Sane yazidi kung'aa Epl


Mshambuliaji wa klabu ya Manchester City, Leroy Sane, amefanikiwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini England wa Oktoba, baada ya kuisaidia timu hiyo kushinda michezo mitatu mfululizo mwezi huo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha kocha Pep Guardiola na amekuwa akipachika mabao mengi pamoja na kupiga pasi za mwisho katika michezo mbalimbali. Katika michezo mitatu ya Oktoba, ameweza kufunga kila mchezo na kutoa pasi ya mwisho.

Kutokana na mabao sita aliyoyafunga mchezaji huyo na kutoa pasi tano za mwisho ndani ya Ligi Kuu, mchezaji huyo ameingia kwenye orodha ya wachezaji wanaotengeneza nafasi nyingi msimu huu akiungna na mshambuliaji wake Sergio Aguero ambaye ana mabao nane na pasi tatu za mwisho.

Katika ushindi wa mabao 7-2 dhidi ya Stoke City, alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya mwisho, huku ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Burnley, alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya mwisho, sawa na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya West Brom.

Sane anakuwa mchezaji wa pili kutoka nchini Ujerumani kuchukua tuzo hiyo, huku mchezaji wa kwanza akiwa Jurgen Klinsmann, ambaye aliwahi kuichukua wakati anakipiga katika kikosi cha Tottenham, Agosti 1994.

Katika tuzo hiyo, Sane alikuwa anashindana na wachezaji watano ambao ni pamoja na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, kiungo Kevin De Bruyne, beki wa klabu ya Arsenal, Nacho Monreal, Glenn Murray kutoka Brighton, kipa wa klabu ya Burnley, Nick Pope na nyota wa klabu ya Crystal Palace, Wilfried Zaha.

“Ninashukuru sana kwa ushirikiano ninaoupata kutoka kwa wachezaji wenzangu, ninaamini kwa hali hii tunaweza kufanya makubwa msimu huu, nawashukuru wote kwa sapoti,” alisema Sane.

Hata hivyo, kutokana na mchango wa Sane ndani ya Man City, amemfanya kocha wake, Guardiola na yeye kuchukua tuzo ya kocha bora wa Oktoba nchini England

No comments:

Post a Comment