Msajili wa Vyama vya Siasa apelekwa Mahakamani na Chama cha ‘Mtikila’
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,Jaji Francis Mutungi.
Chama hicho ambacho kiliasisiwa na Mchungaji Christopher Mtikila ambaye sasa ni marehemu kimewasilisha maombi Mahakama Kuu, kikiomba kibali cha kumfungulia kesi msajili wa Vyama vya Siasa kikimtuhumu pamoja na mambo mengine kuingilia mambo yake ya ndani.
Maombi hayo yaliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dar es Salaam dhidi ya Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) yamepangwa kusikilizwa na Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali, Jumatatu ijayo.
Kwa mujibu wa hati ya maombi ya faragha yaliyowasilishwa mahakamani hapo chama hicho kimefikia uamuzi huo baada ya msajili kukiandikia barua mbalimbali ikiwemo ya kubatilisha mkutano mkuu wa chama uliofanyika Mei 26.
Pia, chama hicho kinapinga hatua ya msajili kutowatambua viongozi wa chama hicho waliochaguliwa katika mkutano huo na badala yake kuwatambua wasio viongozi na wasio wanachama.
Chama hicho kinawakilishwa na mawakili Daimu Halfan na Juma Nassoro.
Kwa kujibu wa hati ya kiapo cha mwenyekiti wa chama hicho, Georgia Mkitila, Aprili 6, msajili alikiandikia barua chama hicho kukikumbusha kuwa uongozi wake ulikuwa unafikia mwisho wake Mei 26, mwaka huu.
Katika barua hiyo, msajili pia alikumbushia chama hicho kufanya mkutano mkuu tarehe hiyo na si vinginevyo.
Georgia, ambaye ni mke wa marehemu Mtikila anaeleza kuwa kutokana na maelekezo hayo ya msajili, chama hicho kiliandaa mkutano mkuu na kikamwandikia msajili barua ya mwaliko.
Anaeleza kuwa msajili alijibu kuwa mkutano huo utakuwa ni batili isipokuwa tu malalamiko yaliyowasilishwa kwake kuhusu uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Georgia anaeleza kuwa Mei 25, chama hicho kilimwandikia barua msajili kutoa maelezo na kusisitiza kuwa mkutano huo utakuwa halali.
Alisema kuwa walifanya mkutano mkuu Mei 26 kwa mujibu wa katiba yao ya mwaka 2002 na kwamba licha ya kumwalika, msajili hakuhudhuria yeye wala ofisa yeyote kutoka ofisi yake.
Alibainisha kuwa baada ya mkutano huo waliwasilisha kwa msajili taarifa zote na mwenendo wa mkutano, ikiwemo orodha ya wajumbe waliohudhuria.
Alifafanua kuwa msajili katika barua yake ya Juni 16, alikiri kupokea taarifa za mkutano mkuu wa chama hicho na kwamba angezitafakari pamoja na malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho ili kujiridhisha.
Georgia alidai kuwa Julai 3, msajili alitangaza kuwa mkutano huo ulikuwa batili na akaamuru chama hicho kiandae mkutano mwingine.
Alisema chama hicho kupitia mamlaka yake ya ndani ya nidhamu kilishamvua wadhifa wa ukatibu mkuu, Feruzi Msimbachaka na kumjulisha msajili,ambaye alikataa kutambua mamlaka hayo ya kinidhamu ya chama.
Alisema msajili amekataa kuwatambua viongozi waliochaguliwa ama kuteuliwa na chama, badala yake anawatambua na kukubali kila kitu kutoka kwa watu walioondolewa madarakani.
No comments:
Post a Comment