Wednesday, 22 November 2017

Meli ya wachina yaibua Matapeli



WAKATI upimaji wa afya bure ukiendelea katika meli maalumu kutoka China, baadhi ya wananchi jijini Dar es Salaam wamegeuza shughuli hiyo kuwa mtaji baada ya kuanza kuuza namba za kadi wanazopatiwa.

Aidha, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Maghembe amesema tayari watu 6,000 wamepata namba kuwawezesha kuwaona madaktari hao kwa utaratibu unaofaa.

Dk Maghembe alitoa mwito kwa wananchi ambao hawajapewa namba, kusubiri hadi waliopata namba hizo watakapohudumiwa. “Tunawaomba msiendelee kusongana; tumeshagawa namba hadi 6,000, hivyo subirini hawa wapate huduma ndipo tutaangalia kama tutaendelea kugawa namba nyingine kulingana na uwezo wa madaktari hawa,”alisema Maghembe.

Meli hiyo yenye madaktari na wataalamu wa afya zaidi ya 380 iliwasili nchini Novemba 19 na inatarajiwa kutoa huduma hiyo kwa siku tano kwa wagonjwa 600 kwa siku. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema amepata taarifa juu ya uwepo wa watu hao wanaofika kwenye meli hiyo kama wagonjwa wanaotaka kuhudumiwa, lakini wakipatiwa namba hizo hugeuka na kuziuza kwa Sh 5,000 hadi Sh 50,000, jambo ambalo ni kosa na kinyume na makusudio.

“Upimaji huo tulisema ni bure na ni makosa kwa mtu kununua au kuuza namba,” alisema. Alibainisha kuwa, baadhi ya wagonjwa wamebainika kutakiwa kusafirishwa kwenda China kupatiwa huduma zaidi hivyo ofisi yake itaandaa utaratibu wa kuwawezesha kusafiri.

Akaongeza, “wagonjwa hawa wanaotakiwa kusafirishwa tutaangalia utaratibu wa kuwasaidia baada ya kupata idadi kamili tutawasaidia kupata hati za kusafiria pamoja na kuangalia utaratibu wa kuwawezesha wakiwa huko kwa matibabu.”

No comments:

Post a Comment