Wednesday, 22 November 2017

Masha afunguka baada ya kuruhusiwa Kurudi CCM Leo


Lawrence Kego Masha, aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema kuwa amefurahi sana kupewa ridhaa ya kujiunga rasmi na CCM leo, Novemba 21, na kwamba atahakikisha anakitumikia ipasavyo.

“Nimefurahi sana kwamba nimepewa ridhaa na mwenyekiti wa Chama  cha Mapinduzi pamoja na Halmashauri Kuu kurejea nyumbani, kurejea CCM. Nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kufuata ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuhakikisha kwamba nakitumikia chama na kulitumikia taifa jinsi inavyotakiwa. Kidumu Chama cha Mapinduzi,” amesema Masha.

Wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu cha CCM kinachoendeshwa na Mwenyekiti wake Rais Magufuli, Masha alieleza kuwa yeye ni kada wa CCM tokea zamani kwani alilelewa na kukulia CCM, hivyo yeye kurudi CCM ni kama kurudi nyumbani na anajuta kufanya maamuzi ya kukihama chama hicho huku akitaka kutumiwa ili kukiendeleza chama hicho na kukiletea maendeleo.

“Mwaka 2015 nilifanya maamuzi ambayo sina sababu ya kueleza sana, nimezaliwa ndani ya chama hiki, nilipohama ilibidi nimfiche mzee Masha, akanipigia simu akanuliza umefanya nini? nikamuuliza kwani wewe chama gani? akaniambia mimi nilifukuzwa we umehama, amefurahi sana juzi nilipomwambia narejea CCM, Mheshimiwa Mwenyekiti na kamati yako, naomba mnikubali, naahidi nitakuwa mwaminifu kwa chama cha Mapinduzi na serikali yake, ukinihitaji nitumie“, amesema Lawrence Masha.

Masha ambaye alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mwaka 2015 akitokea CCM, alitangaza tena kukihama CHADEMA hivi karibuni kwa madai kuwa upinzani hauna nia ya dhati ya kutafuta nafasi ya kuunda serikali, badala yake umejikita katika kuikosoa serikali.

No comments:

Post a Comment