Jaji Mkuu wa Mahakama ya juu zaidi nchini kenya David Maraga
Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya Jumatatu inatarajiwa kutoa uamuzi katika kesi zilizowasilishwa kwenye mahakama hiyo kupinga uchaguzi wa marudio wa tarehe 26 Oktoba ambapo rais wa sasa Uhuru Kenyatta alitangazwa kama mshindi.
Katika Kesi majaji watatakiwa kutoa uamuzi kuhusu masuala yafuatayo:
Wataamua iwapo tume huru ya taifa ya chaguzi na mipaka (IEBC ) ilifaa kuteuwa upya wagombea urais au la.
Uamuzi pia utatolewa na mahakama hiyo juu zaidi juu ya ya ikiwa kujiondoa kwenye uchaguzi huo kwa kiongozi Muungano wa upinzani Raila Odinga na Makamu wake Kalonzo Musyoka kuliathiri uchaguzi huo.
Majaji pia watatoa uamuzi kuhusu ikiwa baada ya tume ya IEBC kushindwa kuendesha uchaguzi katika ameneo bunge 25 kati ya 290 kunahalalisha ama kubatilisha matokeo ya uchaguzi.
Aidha Mahakama hiyo itawaeleza waKenya ikiwa tume ya uchaguzi (IEBC) ilikuwa na uwezo wa kuandaa uchaguzi wa haki na huru baada ya kugubikwa na mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wake.
Kwa upande mwingine Wakenya watasubiri kusikia uamuzi wa mahakama kuhusu kama ghasia zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi wa marudio wa urais ziliathiri ama hazikuathiri matokeo ya uchaguzi na kuufanya kuwa usio wa haki na huru au la.
Mahakama itatoa ufafanuzi juu ya dosari ya karatasi za kupigia kura, maarufu kama form 34A ziliathiri matokeo ya uchaguzi.
Hukumu hii inasubiriwa kwa shauku kubwa na raia wa Kenya pamoja na kwingineko duniani, huku wengio wakijiuliza hatma ya Kenya.
Tangu kufanyika kwa uchaguzi wa marudio wa urais tarehe 26 Oktoba, baadhi ya miji mikuu nchini Kenya ukiwemo mji mkuu Nairobi, pamoja na mji wa magharibi wa Kisumu imekuwa ikikumbwa na ghasia za maandamano ambazo zilizosababisha mauaji ya watu na wengine kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment