Kocha mkuu wa kikosi cha Mbeya City Nsanzurwimo Ramadhani amekubali kubeba lawama kutokana na kipigo cha 5-0 ilichokumbana nacho timu yake ilipocheza ugenini dhidi ya Yanga mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.
Kocha huyo ametoa pole kwa uongozi wa timu yake, wachezaji na mashabiki kutokana na matokeo mabaya ya kupoteza mchezo kwa kufungwa magoli mengi msimu huu Mbeya City ikiwa timu ya pili kuruhusu magoli mengi kwenye uwanja wa Uhuru baada ya Ruvu Shooting kufungwa 7-0 na Simba mwanzoni mwa msimu.
“Nitoe pole kwa Mbeya City kuanzia uongozi wa juu, wachezaji na watu wote, ni vigumu kucheza katika mazingira haya, kama unacheza ligi hii na kufanya makosa yanayopelekea kufungwa magoli mawili ya mapema, lakini kwa upande mwingine pongezi ziende kwa Yanga kwa sababu walitumia vizuri makosa yetu wakatufunga.”
“Mbinu zetu hazikufanikiwa kabisa, hatukucheza vizuri, inaumiza, kwa sababu tulijiandaa vizuri na wachezaji walikuwa na ari kabla ya mchezo lakini wakati wa mchezo zaidi ya asilimia 80 ya wachezaji hawakuwa bora, unategemea nini?”
“Kwa hiyo hatukupaswa kujiandaa? Timu zote zinazojiandaa ni lazima zishinde? Matokeo yaha ni sehemu ya mchezo, hata kama tungeenda Brazil au sehemu yoyote. Timu haikucheza vizuri nakubali na ninabeba mzigo wa lawama kama kocha wa timu, kufungwa goli 5-0 nakubali na ninabeba lawama.”
“Tumepoteza mechi hatujashindwa ligi, bado ligi inaendelea tunarudi kujipanga na kuangalia makosa yetu bado kuna nafasi ya kufanya marekebisho kuona kwa namna gani tutaboresha kiwango chetu.
Ukiangalia utaona kulikuwa na makosa mengi binafsi ya mchezaji mmoja mmoja kuliko makosa kama timu na inatokea kwenye mchezo. Kwa mara nyingine nawapa pole mashabiki wetu.”
No comments:
Post a Comment