Saturday, 3 February 2018

Mkuu wa shule aingia matatani kwa kuchangisha michango



Sumbawanga. Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ameagiza mkuu wa shule ya sekondari Muhama manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa kuchukuliwa hatua kwa tuhuma za kuwatoza wanafunzi michango ya Sh5,000 kama gharama ya kuwapatiwa fomu za maelezo ya kujiunga na shule hiyo.

Wangabo ametoa agizo hilo jana Februari 2, 2018 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Malangali baada ya baadhi ya wananchi kufichua jambo hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Sadock Kalinga amesema wazazi wamekuwa wakichangishwa kiasi hicho cha fedha ili wapatiwe fomu hizo.

“Tulilazimika kutoa fedha hizi na kupewa stakabadhi kwa kuwa tuliambiwa mwanachi ambaye hatotoa fedha  hawezi kupewa fomu hizo na hivyo kukosa sifa ya kujiunga katika shule hii,” amesema Kalinga.

Baada ya kupokea malalamiko hayo na kuonyeshwa risiti iliyotolewa kama ushahidi, Wangabo amemhoji Mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu kuhusu uhalali wa mchango huo ambapo naye alikana kufahamu jambo hilo.

Alimuagiza mkurugenzi huyo kumchukulia hatua mkuu huyo wa shule kwa kuwa kitendo alichokifanya si sahihi kwa sababu Serikali imepiga marufuku michango shuleni.

“Ni marufuku kwa mwalimu yeyote kujihusisha na michango katika mkoa huu. Walimu kazi yao ni kufundisha na sio kuchangisha. Nakuagiza mkurugenzi kuchukua hatua katika hili na ninataka nipate taarifa’,” amesema.

Mwananchi:

No comments:

Post a Comment