Saturday 3 February 2018

Manula, Bocco, Ndemla wapokea tuzo za mwezi


KIPA chaguo la kwanza wa Simba, Aishi Manula amekabidhiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi wa Wekundu wa Msimbazi katika sherehe fupi iliyofanyika juzi  nyumbani kwa Balozi wa Uturuki, Ali Davotuglu.

Manula, ambaye pia ni kipa chaguo la kwanza la timu ya Taifa (Taifa Stars) alishinda tuzo hiyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi nne zilizopita za ligi hiyo inayotarajiwa kuingia kwenye raundi ya pili kuanzia leo.

Mbali na Manula, wachezaji wengine waliopata tuzo katika sherehe hiyo pamoja na nahodha na mshambuliaji aliye kwenye kiwango cha juu, John Bocco na kiungo, Said Ndemla.

"Hizi ni tuzo ambazo zinatolewa na klabu yetu katika kuhamasisha wachezaji wafanye vizuri katika kila mechi wanayocheza na vile vile kusaidia kuipa timu ushindi," alisema Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara.

Aliongeza kuwa katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa klabu hiyo pamoja na mwekezaji na bilionea, Mohamed Dewji "Mo", walifanya mazungumzo mbalimbali na kubadilishana mawazo ili kuifanya timu ifikie malengo yake msimu huu.

"Tunaamini hatua hii tuliyofika, itakuwa na matokeo chanya kwa sababu tutaimarisha mahusiano," Manara aliongeza.

No comments:

Post a Comment