Monday, 29 January 2018

Sh 1.1 Tirilioni zatolewa kusaidia mapambano dhidi ya Malaria


Shirika la Global Fund limetoa ufadhili wa dola za Marekani 525 milioni sawa na Sh1.1 trilioni kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya malaria, kifua kikuu na Ukimwi kati ya mwaka 2018 na 2020.

Kati ya fedha hizo, Sh67 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kifua kikuu zikihusisha elimu kwa wanajamii, vipimo na dawa  kwa watu ambao watabainika kuwa na ugonjwa huo.

Hatua hiyo inalenga kufikia dhamira ya Serikali ya kuwapa matibabu asilimia 70 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2020.

Kuhusu malaria Sh320 bilioni zimetengwa kwa ununuzi wa vyandarua, vipimo (mRDTs) na dawa za kutibu ugonjwa huo.

Kwa mapambano dhidi ya Ukimwi zimetengwa Sh769 bilioni kiasi ambacho Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amekitaja kuwa ni kikubwa kuwahi kutolewa na shirika hilo kwa ugonjwa huo.

Akizungumza leo Jumatatu Januari 29,2018 wakati wa utiaji saini makubaliano ya ufadhili huo, Ummy amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi inayofanywa na wadau wa masuala ya afya.

Waziri Ummy amemhakikishia mwakilishi wa shirika hilo kuwa, Serikali itaongeza usimamizi katika fedha zinazotolewa na wafadhili kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Rais mwenyewe ameniambia kuwa fedha hizi ni nyingi, hivyo tufanye kila linalowezekana kuhakikisha zinatumika kama ilivyoelekezwa, nami naahidi nitazifuatilia kuona zinafanya kazi iliyopangwa,” amesema.

Mwakilishi wa Global Fund nchini, Linden Morris amesema shirika hilo litaendelea kusaidia mapambano dhidi ya maradhi hayo.

Morris amesisitiza wasimamizi wa fedha hizo kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa.
 

No comments:

Post a Comment