Wednesday, 31 January 2018

Wasanii wa filamu watoa msaada wa vifaa tiba

Wasanii wa filamu kutoka taasisi ya ‘Binti Filamu Foundation’ yenye wanawake kumi wa kundi la waigizaji la Bongo Muvi, leo wametoa msaada wa vifaa-tiba vyenye thamani ya Sh. Mil. 30 katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, mmoja wa wasanii hao, Halima Yahya ‘Davina’ alisema:
“Tumejipanga kuwafikia wanawake na mabinti wengi zaidi ili kutoa elimu ya ujasiriamali, kuwaeleza jinsi ya kukabiliana na masuala ya ukatili kwa wanawake na tutajikita zaidi kwenye afya kwani tunaaamini malengo hayo hayawezi kutimia bila afya bora.

“Hivyo tumeamua kuanza na kampeni rasmi katika hospitali tukihamasisha wadau, makampuni na wananchi kwa ujumla kuwekeza katika afya, kuunga mkono juhudi za serikali za awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli yenye kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.

“Binti Filamu Foundation kwa udhamini mkubwa wa Scientific Suppliers pia tumetoa vifaa-tiba vyenye thamani ya Sh. milioni 30 kuunga mkono juhudi za serikali kujali afya ya mama na mtoto.”

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Wilaya ya Kinondoni ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Benjamin Sitta, amesema wasanii wanapaswa kuwa nguzo kubwa katika jamii na wanasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo nchini. Akaongeza kuwa wasanii wengi wana ushawishi mkubwa katika jamii.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo, Mganga Mkuu Mfawidhi katika hospital hiyo, Isdory Kiwale, amesema wanashukuru msaada huo huku akiwahakikishia kuwa vifaa hivyo vitatumika kama vilivyo kusudiwa.

Malengo makuu ya taasisi hiyo ni kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na raia wengine kama vile ukeketaji, ndoa za utotoni, mauaji ya albino na vikongwe na mengine yananyolenga kudhalilisha utu wa mwanadamu.


No comments:

Post a Comment