Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kumuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba na Waziri wa Ardhi William Lukuvi, kufika Siha kutatua tatizo la Kilelepori na wananchi wanaozunguka eneo hilo, endapo Dk. Godwin Mollel atashinda.
Akimnadi Dk.Mollel, katika kata ya Donyomurwak, Katibu wa itikadi na uenezi CCM Taifa, Humphrey Polepole, amesema eneo la Kilelepori ni mali ya Siha, hivyo Chama hicho kikishinda, Serikali itafika ili kuona namna ya kushughulikia mgogoro uliopo kati ya wananchi na eneo hilo la Kilelepori ambalo limekuwa likitumiwa na shule ya Taaluma ya Polisi Moshi (MPA) kwa mazoezi ya kijeshi.
"Natambua mnakabiliwa na changamoto kubwa na eneo la kilelepori, na hii ni kutokana na wananchi kuendelea kuongezeka na mji kupanuka sasa nipeni Dk.Mollel ili Serikali iweze kushirikiana naye kutatua changamoto hii ambayo inawasumbua muda mrefu" amesema polepole.
Polepole amesema siasa za matukio na uongo zimepitwa na wakati hivyo ni vyema wananchi wakatambua Serikali ya chama cha mapinduzi ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia na kutatua changamoto zote zinazowakabili.
Akiomba kura Dk.Mollel aliwaomba wananchi wamchague ili aweze kushughulikia tatizo la maabara kwa shule za kata na kuhakikisha zinakuwa na vifaa ili kuwezesha masomo ya sayansi kusomwa kwa vitendo.
Mollel amesema pia atashughulikia tatizo la maji na kuhakikisha wananchi wa kata ya Donyomurwak wanasambaziwa huduma ya maji safi na salama kwa matumizi ya kunywa, pamoja na kushughulikia tatizo la umeme na migogoro ya Ardhi.
Akiomba kura Mgombea udiwani wa Kata ya Donyomurwak, Lwite Ndosi, ambaye hivi karibuni alijiondoa Chadema na kugombea tena nafasi hiyo kupitia chama Tawala, amewaomba wananchi wamchague tena ili kuweza kushughulika na changamoto zao ambazo ni miundombinu ya barabara, ujenzi wa Bweni la wasichana shule ya Sekondari Sikilari pamoja na ujenzi wa zahanati katika vijiji vilivyopo katika Kata hiyo.
Ndosi ambaye anachuana vikali na aliyekuwa meneja kampeni wake 2015,Sione Mollel (Chadema)alisema akipewa nafasi hiyo, pia atashughulikia mgogoro uliopo baina ya wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka kambi ya Jeshi (Kilelepori) pamoja na kutoa elimu ya mpango mji kijiji cha Munge ambacho kinakua kwa kasi.
"Nimerudi kwa nguvu na kasi mpya, sasa naomba nipeni tena nafasi hii ili niweze kushughulika na changamoto zenu, naahidi pia nitasaidia wananchi ambao wanalalamika maeneo yao kuchukuliwa na Kulelepori ambao ni wa vijiji vya Munge, Emboko, Loiwa na Ormelili"amesema
Akiomba kura mgombea ubunge jimbo la Cuf,Tumsifuel Mwanri, aliwataka wananchi wa Siha kumchagua, kumchagua, kwa kuwa yeye ana msimamo na anaweza kukaa bungeni kuwatumikia wananchi kwa kipindi chote bila kujiuzulu.
Mwanri amesema katika uchaguzi huo mdogo wapo wagombea Wanne wa vyama tofauti Siha, lakini ni jukumu la wananchi wa Jimbo hilo wakachukua maamuzi sahihi ya kumchagua Mgombea wa Cuf ambaye atawatumikia kwa uaminifu.
"Ndugu wananchi, angalieni kiongozi ambaye atawatumikia kwa uaminifu, kwani mkimchagua mwingine anaweza kukaa tena mwaka mmoja na kujiuzulu na kuturudisha tena kwenye uchaguzi" amesema
Mwanri amesema endapo atashinda, pia atashughulikia tatizo la maji na kuhakikisha, gharama zinashuka tofauti na ilivyo sasa ambapo inakuwa mzigo mkubwa kwa wananchi.
Aidha amesema Siha ina ardhi nzuri yenye rutuba lakini haitumiki ipasavyo, hivyo akichaguliwa atashughulika na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kushughulikia tatizo la migogoro na kulipatia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment