Saturday, 3 February 2018

Askari Magereza watiwa mbaroni wakidaiwa kuua

KAMANDA WA POLISI MKOA WA TANGA, EDWARD BUKOMBE.

ASKARI 12 wa Jeshi la Magereza wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wanahojiwa na polisi kwa tuhuma za mauaji yaliyochochewa na ugomvi wa mapenzi.

Askari hao wanadaiwa kumshambulia mkazi wa kijiji cha Kerenge wilayani hapa, Aloys Makalla na kusababisha kifo chake mwishoni mwa mwezi uliopita huku wakiwa wamevaa kininja.

Katika tukio hilo ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, imedaiwa kuwa saa chache kabla ya kifo chake, marehemu alikuwa amepigana na mmoja wa askari.

Kamanda Bukombe alisema tukio hilo lilitokea Januari 28 na kwamba askari 12 wa Magereza wanahojiwa na polisi katika upepelezi wake.

“Ni kweli tumepata taarifa za tukio hilo la mauaji ya mwanakijiji huyo na askari 12 tunawachunguza kupata ukweli wake, ili kuona kama kuna wanaohusika hatua ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Kamanda Bukombe.

Akihadithia mkasa wa mauaji hayo, mkazi wa kijiji cha Kerenge, Juma Salim, alisema marehemu alikuwa na mzozo wa muda mrefu na askari Magereza mmoja (jina tunalihifadhi) wakituhumiana kuingiliana katika penzi la mmoja wa wanawake kijijini hapo.

"Na siku hiyo (mzozo huo) ulizusha vurugu kubwa," alisema Salim.

Salim alisema katika ugomvi huo kati ya askari na Makalla, Magereza huyo alijeruhiwa na kurudi kwenye makazi yao lakini baada ya muda alirejea kijijini hapo na wenzake wakiwa wamevalia kininja na kuwapiga wenyeji.

Baadaye walimkamata Makalla waliyemtuhumu kumpiga mwenzao na kuondoka naye, alisema Salim.

Naye Jeniffer Leonard, mkazi mwingine wa Kerenge alisema askari hao waliondoka na Makalla kwa madai ya kumpeleka kituo cha polisi lakini walishangaa kupata taarifa za kifo chake baadaye.

HAKUMTAJA JINAAkielezea tukio hilo, Kamanda Bukombe alisema taarifa zinaonyesha kutokea ugomvi baina ya askari ambaye hata hivyo hakumtaja jina wala cheo chake na marehemu huyo, hali iliyosababisha Magereza kujeruhiwa.

Bukombe alisema baada ya kujeruhiwa, askari huyo alikwenda kambini kuchukua wenzake ambapo walirudi kwa mara ya pili na kumkamata marehemu, kumpakia kwenye gari na kuondoka naye kwa madai ya kumpeleka kituo cha polisi.

Kamanda Bukombe alisema taarifa kutoka kwa askari Magereza zinadai wakati wakiwa njiani, marehemu aliruka kutoka kwenye gari hiyo na kuanguka barabarani ambako alifikwa na mauti.

“Tunachunguza upi (ndiyo) ukweli wa marehemu," alisema Kamanda Bukombe. "Kauawa kwa kipigo cha askari hao ama (ni) kifo kinachotokana na kuanguka kwa kuruka kwenye gari."Mambo hayo ndiyo tunayoyachunguza tupate ukweli.”

Alisema matokeo ya uchunguzi huo ndiyo yatakayoamua kama kuna hoja na ukweli kwamba askari wamehusika na kifo cha marehemu na hatua zitachukuliwa, ikiwemo kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote.

No comments:

Post a Comment