Saturday, 3 February 2018

Nduda, Mbonde njiani kurejea dimbani

Mlinda mlango namba mbili wa Simba, Said Mohammed 'Nduda' wiki ijayo anatarajia kujiunga na wenzake tayari kuanza mazoezi baada ya kuwa nje kwa miezi mitano, kufuatia kufanyiwa upasuaji wa goti Oktoba mwaka jana nchini India.

Nduda aliyesajiliwa na klabu ya  Simba Julai mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, hajacheza mechi yoyote msimu huu kutokana na maumivu ya goti aliyoyapata Agosti mwaka jana mazoezini akiwa visiwani Zanzibar wakati Simba inajiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga Agosti 23, mwaka jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Kwa sasa mlinda mlango huyo ameanza programu za mazoezi yake binafsi tangu mwanzoni mwa mwaka huu, akijifua ufukweni kwa mazoezi.

Wakati huo huo, beki wa kati wa Simba, Salim Mbonde anaendelea na mazoezi ya gym baada ya kuwa nje kwa zaidi ya miezi mitatu kufuatia kuumia Oktoba 15, mwaka jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya timu yake ya zamani, Mtibwa Sugar uliomalizika kwa sare ya 1-1 mjini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment