Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetoa mpangilio wa ubora wa ufaulu kimikoa wa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017, huku Dar es Salaam ukikosekana katika mikoa 10 iliyofanya vizuri.
Hata hivyo, mkoa huo umepanda kutoka nafasi ya 18 mwaka juzi, hadi nafasi ya 16 mwaka jana. Katika orodha hiyo mkoa wa Kilimanjaro umepanda kutoka nafasi ya tano mwaka 2016 hadi nafasi ya kwanza mwaka jana.
Mkoa wa Pwani nao umepanda kutoka nafasi ya saba mwaka juzi hadi nafasi ya pili mwaka jana. Katika orodha hiyo Tabora imeshika nafasi ya tatu kutoka nafasi ya 10 mwaka 2016.
Mikoa mingine iliyofuata na nafasi iliyoshika ni Shinyanga (nafasi ya nne kutoka nafasi ya tisa), Mwanza (nafasi ya tano kutoka nafasi ya sita).
Mkoa wa Njombe uliokuwa kwa kwanza mwaka 2016, mwaka jana umeporomoka hadi nafasi ya 15.
Mkoa wa Iringa ulishika nafasi ya pili mwaka 2016, lakini mwaka jana umeporomoka hadi nafasi ya 17 huku Kagera ulioshika nafasi ya tatu, ukishuka hadi nafasi ya tisa.
Mkoa ulioshika mkia katika mpangilio huo ni Kaskazini Unguja uliotoka nafasi ya 29 mwaka juzi hadi nafasi ya 31 mwaka jana, ukifuatiwa na Kusini Unguja ulioshika nafasi ya 30 ambayo pia uliishika mwaka juzi.
Mikoa mitano iliyoshika mkia ni Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na Lindi.
No comments:
Post a Comment