Tuesday, 30 January 2018

Mshindi wa pili kidato cha nne amtaja Mungu na wazazi wake


Elizabeth Mangu, mshindi wa pili Kitaifa katika mitihani ya kidato cha nne  amesema kumtanguliza Mungu katika kila kitu  ndoto ya kuwa wa kwanza, bidii kwenye masomo na usimamizi wa karibu wa wazazi na walimu ndiyo  siri ya mafanikio yake.

Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Mwanza leo Januari 30, Elizabeth amesema  tangu alipojiunga kidato cha kwanza, alijiwekea lengo la kushika nafasi ya kwanza katika mitihani ya Taifa na aliwafuata walimu wake kuomba ushauri wa kufanikisha lengo hilo.

“Niliweka lengo la kushika nafasi ya kwanza kama alivyofanya Robina aliyeongoza mitihani ya kitaifa akitokea shule yetu ya Marian Girls; nilimfuata Mwalimu wa taaluma Ihonde na mwenzake wa Civics anayeitwa Mwanduzi kuwaomba ushauri wa kufanikisha hilo,” anasema na kuongeza

“Wote walinishauri kuzingatia masomo, kusoma pamoja na kusaidia wenzangu darasani kama njia ya kujifunza, kuzingatia maelekezo ya walimu na wazazi shuleni na nyumbani pamoja na kumcha Mungu kama mwanzo wa hekima,”

Akizungumza mbele ya mama yake mzazi, Wande Mandalu ambaye ni mwalimu katika shule ya Sekondari ya Kiloleli jijini Mwanza, Elizabeth alisema mwongozo na ukali wa wazazi wake aliposhuka kitaaluma pia imesaidia mafanikio yake.

“Nawashauri wazazi wawe karibu na kufuatilia mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani hadi shuleni na kuwatia moyo wanapofanya vema bila kuacha kuwaonya na kuwakaripia wanapokosea,” amesema

Kauli hiyo iliungwa mkono na mama yake, Wande Mandalu pamoja na Mwalimu wake wa masomo ya dini katika Kanisa la KVCC, Geofrey Lugwisha waliosema liha ya kuwajenga watoto katika imani ya kiroho, wazazi wana wajibu wa kuwasaidia watoto wao kielimu, kuwapongeza na kuwaonya wanapopotoka.

“Wazazi lazima tuwe wasimamizi wa karibu kwa kufuatilia nyendo za watoto kuanzia nyumbani, shuleni hadi mitaani; lazima wajua ratiba na kuwapa miongozo inayofaa maishani, hasa msisitizo kwenye elimu ambayo ndio urithi wa kudumu,” amesema  Mwalimu Mandalu, mama wa watoto watatu

Eliza ni mtoto wa pili katika familia yake ya watoto watatu akitanguliwa na kaka yake Joseph Mangu na mdogo wake, Carren Mangu aliyesoma kidato cha kwanza shule ya wasichana ya Marian.

No comments:

Post a Comment