Wagombea ubunge jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia (CCM) na Salum Mwalimu (Chadema) wameendelea kujinadi katika mikutano ya kampeni, huku Mtulia akiwashangaa wanaobeza kujiondoa kwake CUF na kujiunga na chama tawala.
Wakati Mtulia akimwaga sera leo Jumatatu Januari 29, 2018 katika uwanja wa Hananasif Kinondoni, Mwalimu alikuwa uwanja wa Mtambani kata ya Mzimuni.
Tangu kuanza kwa kampeni hizo, hoja ya hamahama ya madiwani na wabunge imekuwa ikitawala kutokana na CCM kujikita kuzungumzia sababu za mgombea wake wa Kinondoni, Mtulia kuteuliwa kuwania tena nafasi hiyo, huku Chadema wakitumia kete hiyo kumnadi Mwalimu.
“Nyalandu (Lazaro-aliyekuwa mbunge Singida Kaskazini) na Godwin Mollel (Siha) nao walihama vyama vyao lakini mimi ndiye nazungumzwa sana na kusema kila chama kimepoteza mbunge wake lakini kuna chama kimeumia kuliko vingine,” amesema na Mtulia.
Amesema, “Wakati nikiwa upinzani sikuwa na namba ya Rais, sasa ninayo mkiwa na matatizo mnaniambia mimi nampigia na mambo yanatekelezwa. Kama kawaida yake yuko kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wote bila ubaguzi.”
Kama ilivyo kwa Mtulia, Dk Mollel naye alikuwa mbunge wa Chadema jimbo la Siha lakini Desemba 14,2017 alihamia CCM na kupitishwa kuwania ubunge huku Nyalandu ambaye alikuwa mbunge kwa tiketi ya CCM, alihamia Chadema.
Akizungumza katika kampeni hizo Mtulia amesema, “Nitakuwa mbunge wa chama dola na ninakwenda kutekeleza ilani ya uchaguzi, mtu yeyote asijaribu kuzuia ilani hii kutekelezwa. Naomba kila mmoja awe mwakilishi wangu wa kuniombea kura. Ukichagua Mtulia umechagua maendeleo.”
Akiomba kura, Mwalimu alisema, “Naahidi kwenda kuwa mbunge wa kuwatumikia wananchi wote si Chadema tu. Siendi kuwa mbunge mnafiki, nitatumia talanta zote na ninaahidi makazi bora Kinondoni, kuna changamoto ya mafuriko.”
Mwalimu amesema, “Naahidi tutatenga fedha kuondoa mafuriko. Kuna tatizo kubwa la afya, tuna kata nne tu zenye zahanati na kituo kimoja cha afya. Napaswa kusimamia afya. Naenda kusimamia, hakuna bodaboda wala mama ntilie atakayenyanyaswa.”
No comments:
Post a Comment