Baada ya Halmashauri ya Kigambini kugawanywa mwaka juzi kutokea Temeke, Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo limekutana na kupitisha sheria ndogo tisa ambazo zitatumika kuendesha halmashauri hiyo.
Sheria hizo mpya ambazo ndani yake kuna kanuni ni sheria ndogo za ushuru na huduma, ada na ushuru, matangazo, maegesho, uvuvi na rasimali za bahari ya hindi, masoko na magulio, usafi wa mazingira, burudani na sheria ya kudumu ya halmashauri.
Madiwani hao wamepitisha sheria hizo katika kikao chao cha pili cha robo cha baraza hilo kilichokuwa na ajenda 10 ikiwemo kupitisha sheria hizo na kanuni zake ili kuachana na sheria zilizokuwa zikitumika hapo awali ambazo zilikuwa ni za Halmashauri ya Temeke kabla ya kutenganishwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Stephen Katemba alisema mchakato wa kubadilisha sheria na kanuni hizo umepitia ngazi mbalimbali ikiwemo kushirikisha wadau na wananchi kuanzia ngazi ya mtaa hadi ya kata.
" Hizi sheria zikianza kutumika lazima wananchi watambue kuwa zitakua na adhabu kwa wale ambao watazikiuka, na faini ya makosa yake itaanzia Sh 200,000 hadi Milioni moja punde tu ambapo sheria na kanuni hizi zitaanza kutumika miezi michache ijayo," Alisema Katemba.
No comments:
Post a Comment