Saturday, 2 December 2017

Mbao FC waitwa mezani na Mshambuliaji wa Stand


Wakati Mbao FC ikiwa na tatizo katika safu ya ushambuliaji, mshambuliaji wa Stand United, Omary Kanyoro amesema yupo huru kuzungumza na timu yoyote inayotaka huduma yake.

Mbao imekuwa na tatizo katika safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikikosa mabao ya wazi katika msimu huu wa Ligi Kuu.

Kanyoro alisema kwa sasa yuko huru kujiunga na klabu yoyote kwani msimu huu hakusajili Stand United katika dirisha kubwa la usajili.

Alisema anatamani kuchezea klabu ya Mbao ambayo katika msimu wa 2016/17 alitaka kusajiliwa, lakini Stand United wakapanda dau kuwazidi wachana Mbao hao wa jiji la Mwanza.

“Mbao ni timu nzuri na kwa sasa natamani kwenda kuchezea kwani ina kocha mzuri hivyo kama wakija basi nipo tayari kujiunga nao”alisema Kanyoro.

Hata hivyo Mshambuliaji huyo alisema pia anakaribisha ofa kwa klabu mbalimbali za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza ambapo yeye yuko tayari kukipiga iwapo watahafikiana kwenye maslahi.

“Sikuweza kusaini mkataba mpya na Stand United katika dirisha kubwa la usajili kutokana na sababu mbalimbali lakini kwa sasa niko huru hivyo klabu yoyote nakaribisha ofa zao,”alisema mshambuliaji huyo.

No comments:

Post a Comment