Saturday, 3 February 2018

Wanaofanya udanganyifu kwenye asasi za kiraia waonywa

Asasi za kiraia zimetakiwa kufuata taratibu kabla ya kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi ili kukwepa udanganyifu, ikiwa ni pamoja na kuwachangisha fedha na kutokomea kusikujulikana.

Kauli hiyo imetolewa leo Februari 3, 2018  na ofisa maendeleo ya jamii Manispaa ya Temeke, John Bwana wakati akizindua  mradi wa kuwajengea wanawake uwezo kuhusu ujasiriamali ili  kujiinua kiuchumi ulioandaliwa na asasi ya Iwapoa.

Amesema kuna lundo la asasi za kiraia zinazotoa mafunzo kiholela na kuwatapeli wanawake kwa kuwachangisha michango na kutokomea na fedha zao.

“Iwapoa mmefanya jambo la maana kufuata taratibu za kuonana na mamlaka husika na kupata wataalamu kutoka katika kata mtakazofanya kampeni hii ya kupunguza umasikini kwa kuwajengea wanawake uwezo,|” amesema na kuongeza,

“Nawaunga mkono na ninatoa rai kwa asasi nyingine zisizofuata utaratibu zifanye hivyo mara moja kwa sababu tunazifuatilia na tukizibaini tutazizuia kufanya kazi zake katika maeneo yetu.”

Mratibu wa  mradi huo kutoka Iwapoa,  Yusuph Kutegwa amesema mradi huo utatekelezwa katika kata sita za Manispaa ya Temeke.

Amezitaja kata hizo kuwa ni Buza, Keko, Chamazi, Vituka, Azimio na Charambe.

Amesema utawafikia wanawake 150 kutoka katika maeneo hayo waliyoyachagua kutokana na kuwa na wingi wa watu, wakiwamo wanawake wasiokuwa na shughuli za kudumu.

“Ili kuwapatia masoko na mitaji tutawaunganisha katika vikundi vya watu watano watano, ili iwe rahisi kuwapa ujuzi kwa pamoja, ”amesema Kutegwa.

No comments:

Post a Comment