Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Jerusalem lililopo Kitunda jijini Dar, Nabii James Nyakia amesimulia alivyonusa kifo baada ya kutekwa na kuteswa kwa siku kadhaa na watu wasiojulikana.
Tukio hilo la kutisha lilimtokea nabii huyo mwaka jana alipokuwa akitangaza Injili huko Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza na gazeti hili katika kanisa hilo baada ya kukimbia huko, Nabii Nyakia alisema kuwa, alikuwa katika program ya kutangaza habari njema wilayani humo ndipo siku moja akakutana na kundi ambalo baadaye alisikia ndilo lile la watu wasiojulikana ambao walimkamata akiwa msituni na kuanza kumtesa.
“Nilikuwa nimeamua kwenda kupeleka neon la Mungu vijiji mbalimbali vya Mkuranga.
“Nakumbuka siku moja nilikuwa katikati ya msitu mkubwa kwani Mkuranga imezungukwa na mapori na misitu.
“Nikiwa njiani kwenda kufanya mkutano wa Injili, ghafla walitokea vijana waliokuwa na silaha za kijadi kama marungu na mapanga. Pia kulikuwa na wachache waliokuwa na bunduki.
“Walinieleza kuwa hawakutaka kusikia habari za kueneza injili kwani walisema wao wanataka dini yao tu na nadhani walishanijua kwa sababu muda mwingi kazi hii ya Mungu niliifanyia huko.
“Niliwaomba sana wasiniue, lakini cha moto nilikiona maana kama ni kupigwa, nilipigwa sana. Kwa kifupi mateso hayakuwa ya kawaida.
“Nilichokifanya ilikuwa ni kumuomba Mungu kimoyomoyo na kumwita aniokoe au anipokee mikononi mwake kwani niliamini kama ni kufa, ningekufa nikiwa ninaitenda kazi ambayo Mungu ameniita kwayo.
“Baada ya maombi na mateso ya saa zaidi ya sita, wale jamaa nilisikia wakiambizana kwamba waliachie, lakini kwa onyo kwamba nisiendelee na shughuli hiyo.
“Waliponiachia nilirejea kwa mwenyeji wangu, lakini tulizidi kumwomba Mungu hadi tuliposikia baadhi yao walikamatwa na polisi na wengine kuuawa na sasa kuna utulivu wa kutosha,” alisema Nabii Nyakia akiwa na makovu ya mateso hao kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake.
No comments:
Post a Comment