Saturday, 3 February 2018

Kauli ya kocha wa Simba yamwacha mdomo wazi Tambwe


KAULI ya Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, aliyedai kwamba atafurahi zaidi kama straika wake Emmanuel Okwi atafunga mabao 30 msimu huu, imemshitua mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe.

Tambwe ambaye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu wa 2015/16 akifunga mabao 21, baada ya kusikia kauli hiyo ya Djuma alisema; “Siyo kazi rahisi Okwi kufunga mabao 30.”

Akizungumza na Championi Jumamosi, Tambwe alisema ili Okwi ambaye hivi sasa anaongoza kwa ufungaji akiwa na mabao 12, aweze kufikisha mabao 30, anatakiwa kufunga katika kila mechi atakayocheza.

“Siyo kazi rahisi kwa Okwi kufunga mabao 30, kwani mzunguko wa pili ligi huwa ni ngumu sana, kila timu hupambana kuhakikisha inafanya vizuri ili kuwania ubingwa, nyingine zinapambana zisishuke daraja.

“Inabidi Okwi apambane kwelikweli na ajitahidi pia kufunga katika viwanja vya mikoani lakini kama ataendelea kutegemea Uwanja wa Uhuru na ule wa Taifa pekee, itakuwa ni vigumu kufikisha mabao hayo,” alisema Tambwe.

No comments:

Post a Comment