MWALIMU wa Shule ya Msingi Makazi Mapya, Kata ya Malangali Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, ameihama nyumba aliyokuwa akiishi ili kupisha wanafunzi waitumie kama darasa.
Mwalimu huyo, amelazimika kufanya hivyo kutokana na shule hiyo kutokuwa na vyumba vya madarasa vya kutosha.
Akizungumza na gazeti hili jana, Diwani wa Kata hiyo, Anthony Chomo, alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2003 lakini ina changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa.
Chomo alisema mwalimu huyo amehama katika nyumba ya shule aliyokuwa akiishi ili wanafunzi wa darasa la awali wapatao 51, waitumie kama darasa.
Alisema kutokana na uhaba huo wa vyumba vya madarasa, wanafunzi wa darasa la kwanza ambao idadi yao ni 101 pamoja na wengine 67 wa darasa la tatu, wanalazimika kusoma kwa zamu katika chumba kimoja kwa zamu za asubuhi na mchana.
Diwani Choma alisema kutokana na changamoto hiyo, walimwomba Mbunge wa Sumbawanga Mjini fedha na kuwapatia Sh. milioni tatu kutoka katika Mfuko wa Jimbo na wameanza ujenzi wa vyuumba vya madarasa ili kutatua tatizo hilo.
Choma alisema wamekwishafikisha suala hilo kwenye uongozi wa Halmashauri ya Manispaa na wanaendelea kusubiri licha ya kuwa imekuwa muda mrefu na mpaka sasa wanafunzi wanasoma kwa shida na walimu wanafundisha kwa shida pia.
Alisema iwapo jitihada hazitafanyika haraka kujenga madarasa, wanafunzi hawatakuwa na uelewa mzuri kutokana na kusoma kwa shida na walimu pia ufundishaji wao utakuwa hauna kiwango kinachotakiwa, hivyo lengo la serikali la kila mwanafunzi kupata elimu bora litakuwa halijafikiwa.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu, alisema manispaa inasubiri wananchi waanze nguvu kazi ya ujenzi wa madarasa katika shule hiyo ndipo wasaidie umaliziaji.
Njovu alisema iwapo wananchi watatekeleza wajibu huo, shule hiyo itapata madarasa upesi zaidi kwa kuwa halmashauri imepokea fedha kutoka mradi wa kuimarisha elimu ujulikanao Kama P4R, hivyo fedha hizo zitatumika katika kuboresha mazingira ya elimu ya shule hiyo.
Hata hivyo, Njovu alimwomba diwani huyo kuwahimiza wananchi ambao watoto wao wanasoma katika shule hiyo, kuhakikisha wanajituma katika kuboresha mazingira ya elimu ya watoto wao baada ya kukaa na kusubiri wahisani na serikali kwa kuwa yale yaliyo ndani ya uwezo wao, wanapaswa kuyafanya kwa maslahi ya elimu ya watoto wao na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment