Monday, 29 January 2018

Baada ya vichapo Mbao FC kujiuliza kwa Kariakoo ya Lindi


Baada ya kuchezea vichapo viwili mfululizo katika Ligi Kuu kwa Mbao FC, sasa imepanga kufanya kweli katika mchezo wao wa kombe la FA dhidi ya Kariakoo Lindi utakaopigwa Jumatano hii.

Wababe hao wa vigogo wa Ligi Kuu Simba na Yanga, walichezea vipondo mechi zao mbili bila majibu,ambapo walianza kulizwa na Stand United bao 1-0 wakiwa nyumbani, kisha kuchapwa tena na Ruvu Shooting mabao 2-0 ugenini.

Nahodha kikosi hicho,Yusuph Ndikumana alisema wanawafuata Kariakoo kwa lengo moja tu kusaka ushindi ili kusonga mbele kwenye mashindano hayo.

Alisema makosa waliyoyafanya katika mechi zao za Ligi Kuu hawatarajii yajirudie na kwamba wanahitaji kutwaa ubingwa huo ambao waliukosa msimu uliopita.

“Tunaenda kwa lengo moja la kusaka ushindi ili kusonga mbele,ni mchezo mgumu na muhimu sana kwetu,makosa tuliyoyafanya hatutarajii kuyarudia kwenye FA”alisema Ndikumana.

Beki huyo aliongeza kuwa Kariakoo hawaijui kiundani, hivyo watakuwa makini kuzuia aina yoyote ya mashambulizi langoni mwao kuhakikisha hawapiti kirahisi ili kufikia malengo yao.

“Hatuwajui Kariakoo, kwahiyo tutakuwa na tahadhari sana nao kuwakabili, tunalenga sana kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kuukosa msimu uliopita”alisema nahodha huyo Mrundi.

Mbao ilifanikiwa kufika fainali ya mashindano hayo katika msimu uliopita na kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Simba, ambayo tayari imeshayaaga mashindano hayo.


No comments:

Post a Comment