Saturday, 3 February 2018

Yanga yajihakikishia ushindi dhidi ya Lipuli leo



KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, amesema kama watashindwa kupata ushindi kwenye mchezo wa leo dhidi ya Lipuli ya Iringa watajiweka pabaya katika kuutetea ubingwa wao msimu huu.

Lwandamina, alisema kuwa kwenye mchezo wa leo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, wana kila sababu za kuhakikisha wanapata ushindi ili kuendelea kuifukuzia Simba inayoongoza ligi.

Yanga itaingia kwenye uwanja huo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 18 tangu Lipuli ilishuka daraja mwaka 1999 na kuwafanya mashabiki wa mkoa wa Iringa kushindwa kuziona timu kubwa na kongwe zenye mashabiki wengi, ikiwemo Yanga.

“Ni mchezo mgumu kama ilivyo michezo mingine, tupo ugenini lakini kwa namna mambo yalivyo ni lazima tupambane ili kutoongeza pengo la pointi na wanaoongoza ligi,” alisema Lwandamina.

Yanga imeachwa kwa pointi saba na Simba wenye pointi 35 huku Azam wanaoshika nafasi ya pili wakiachwa kwa pointi tano na vinara hao, kikosi cha Lwandamina kinashika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 28.

Mchezo wa leo utamshuhudia mshambuliaji Ibrahim Ajibu akirejea uwajani baada ya kuukosa mchezo wa kombe la FA dhidi ya Ihefu, muunganiko wake na Obrey Chirwa unatazamiwa kuwa chachu ya ushindi kwa mabingwa hao watetezi.

Canavaro anena

Kuelekea kwenye mchezo wa leo, nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Canavaro’, amesema watahakikisha wanapambana mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha wanapata ushindi.

“Tulitoka sare kwenye mchezo wetu wa kwanza Dar es Salaam, hiyo inaonyesha Lipuli si timu ya kuibeza, kama wachezaji tutahakikisha tunakuwa makini na kupambana muda wote,” alisema Canavaro.

Naye kocha wa Lipuli, Selemani Matola, aliiambia Nipashe kuwa wamejiandaa vyema kuwakabili mabingwa hao watetezi.

No comments:

Post a Comment