Tanga. Naibu waziri na mkuu wa mkoa katika Serikali ya Awamu ya Nne, Mwantumu Mahiza amejichimbia katika kilimo cha muhogo.
Mahiza aliyekuwa naibu waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi na mkuu wa mikoa ya Tanga, Pwani na Lindi amewahamasisha wananchi kulima zao hilo akisema litawapa utajiri wa haraka.
Kwa sasa Mahiza amejikita kulima muhogo katika Kijiji cha Segera wilayani Handeni mkoani Tanga akisema soko la bidhaa hiyo lipo ndani na nje ya nchi.
Akizungumza wakati wa kongamano la wanawake Mkoa wa Tanga jana Jumanne Novemba 21,2017 amesema wazo la kulima muhogo alilipata akiwa naibu waziri baada ya kuona Rais na waziri mkuu wakijihusisha na kilimo.
“Nilimtembelea Rais kwa wakati ule, Jakaya Kikwete nikakuta muda wake wa mapumziko anautumia shambani na anazalisha mazao mbalimbali, nikaenda kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pia hali ikawa vivyo hivyo. Nikaona kama Rais na mawaziri wakuu wanalima ni kwa nini mimi nisilime?” amesema Mahiza.
Amesema aliamua kwenda kijijini kwa mumewe kuanzisha kilimo cha mazao mbalimbali na baadaye akajikita kulima muhogo.
“Kwa eka moja kuanzia kuandaa shamba, kupanda na kupalilia unaweza kutumia gharama ya Sh450,000 kama hatua zote unafanyiwa na vibarua. Hadi kukomaa inachukua kati ya miezi minne na tisa kulingana na aina ya mbegu, lakini ukivuna na kuuza unajipatia Sh4 milioni, unataka nini tena?” amehoji Mahiza.
Ametaja aina ya mihogo anayolima na kuuza ndani na nje ya nchi kuwa ni kiroba, mzurikwao, mahiza, kibandamaiti na mpemba ambazo mbali ya kutumika kwa kukaangwa na unga; kuna viwanda vinavyozalisha dawa za binadamu, biskuti, tambi, mikate na vyakula vya mifugo.
Mahiza ameishauri Serikali kuweka programu maalumu ya kuwahamasisha vijana na wanawake kutumia asilimia tano zinazotolewa na halmashauri kupitia makusanyo ya ndani kuzalisha muhogo kwa sababu anafahamu China inahitaji zao hilo kutoka Tanzania na uzalishaji kwa sasa hautoshelezi mahitaji.
Mwenyekiti wa baraza la wanawake Mkoa wa Tanga lililoandaa kongamano hilo, Mariam Shamte ametaka wanawake kwenda shambani kwa Mahiza kujifunza kilimo hicho.
Pia, ameziomba taasisi za fedha kuchangamkia mikopo ya uzalishaji wa muhogo kwa sababu ni zao la muda mfupi.
No comments:
Post a Comment