Singida. Serikali imesema haijatoa ruhusa Chuo Kikuu Huria (OUT) kiendelee kutoa kozi ya ‘Foundation’ kama ambavyo imedaiwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii.
Baadhi ya mitandao imetoa taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho: “Waziri Mkuu aruhusu kozi za 'Foundation' Chuo Kikuu Huria” kwa madai kuwa alitoa ruhusa hiyo jana (Alhamisi, Novemba 30, 2017) wakati akiwa mkoani Singida ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu hicho.
Akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Singida waliohudhuria mahafali ya 33 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini Singida, Waziri Mkuu amesema Serikali bado inafanyia maboresho Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014.
“Kwa sasa Serikali inafanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo kwani sera tuliyonayo haifafanui vizuri jinsi ya kuwasaidia vijana wetu wajiendeleze kwa njia ya mfumo wa elimu huria na masafa,” amesema
“Programu kama zilizoelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo za Foundation, zinahitaji pia kufafanuliwa kwenye sera yetu, ambayo kwa sasa wataalamu wetu wanaendelea kuiboresh’’amesema
Ameongeza kwamba ‘’ Pindi itakapokamilika, tutaitolea taarifa kwa Chuo Kikuu Huria na wataalamu wataweza kushirikiana na sekta zote ili kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri,” amesema
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Tozo Bisanda amesema wamepokea barua kutoka kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwaarifu juu ya nia ya Serikali kutaka kurejeshwa kwa kozi za Foundation katika chuo hicho.
“Tayari tumekwisha wasilisha mtaala wa Foundation ulioboreshwa ili kukidhi matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), na tunasubiri mrejesho kutoka Kamisheni baada ya kikao chao, mapema mwezi ujao,” amesema Prof. Bisanda.
No comments:
Post a Comment