Friday 1 December 2017

Kampuni ya Ford kuachana na magari ya zamani

BOSI mpya wa kampuni ya magari aina ya Ford ya Marekani, ametangaza kuingia katika mpango wa kushindana katika soko kwa kuachana na aina ya magari iliyozoea kuzalisha ‘miaka nenda rudi.’

Bosi huyo, Jim Hackett, katika mikakati yake anasema analenga katika magari ya mfumo mpya unaoegemea zaidi matumizi ya umeme.

Hackett anasema, pia kampuni hiyo kupitia uzalishaji huo na mikakati mingi inatarajiwa kupunguza gharama za uzalishaji kwa wastani wa Dola za Marekani bilioni 14.    Mtendaji huyo mkuu anasema ni maamuzi yaliyofikiwa, baada ya kufanyika tathmini ya siku 100 kuhusu uzalishaji na hali ya soko.

Hackett aliingia ofisini mwezi Mei mwaka huu, akichukua nafasi ya mtangulizi wake Mark Fields, aliyedumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu.

Inaelezwa kwamba, katika zama za Mark licha ya kampuni kupata faida kubwa, lakini nafasi yake katika soko la magari kimataifa ilianguka sana.

Wataalamu wa masoko kimataifa wanasema nafasi ya Ford, ambayo ni kampuni ya Kimarerkani imeshuka katika soko kutokana na ushindani wa kimataifa hasa kutoka  kwa Wachina na mataifa mengine yanayoibuka.

Hackett anasema, wana mpango wa kuhakikisha asilimia 90 ya magari yanayozalishwa yanaingia katika masoko mbalimbali duniani kuchukua nafasi kubwa ya mauzo, hadi ifikapo mwaka 2020.

Pia, katika muundo magari yanayotarajiwa kuingia sokoni itakuwa na vifaa vingi ndani yake kama vile simu, yote ikilenga kumvutia mteja.

Mengine yanayolengwa na kampuni ni maboresho ya kuzalisha magari ya biashara, wagonjwa na mabasi ya abiria Marekani na kwingineko na tayari bosi huyo anasema wameshaingia mkataba na baadhi ya kampuni kuifanya kazi hiyo.

Hackett anasema huko nyuma walisuasua kuingia katika ushindani wa kuweka mfumo wa umeme kwenye magari wakihofia gharama kubwa, lakini sasa Ford imeamua kujitosa katika aina hiyo ya magari ambayo ndio mvuto wa soko uliopo duniani.

Katika kuanzisha hilo, Ford iliingia mkataba na kampuni za kichina kuzalisha magari hayo ya umeme, ikizingatia Wachina walishapiga hatua sokoni na katika uzalishaji.

No comments:

Post a Comment